TEHRAN: Iran itaanzisha upya harakati za kinyuklia
10 Mei 2005
Iran imesema kuwa itaanzisha upya harakati za kuimarisha madini ya uranium katika muda wa siku chache zijazo.Mjini Tehran,makamu wa mkuu wa miradi ya kinyuklia ya Iran,Mohamed Saeedi amesema mtambo wa Isfahan utaanza kufanya kazi tena.Serikali ya Iran mwaka jana katika hatua ya kutaka kuwaonyesha wapatanishi kutoka Umoja wa Ulaya nia yake nzuri,ilisitisha kuzalisha nishati ya kinyuklia katika mtambo huo.Ujerumani,Ufaransa na Uingereza zimekuwa zikiendesha majadiliano pamoja na Iran na kutoa vichocheo vya kiuchumi kuishawishi Iran isitishe mipango yake yote ya kinyuklia.Marekani inayoituhumu Iran kuwa inajaribu kutengeneza silaha za kinyuklia,imeonya kuwa hatua yo yote ile ya kuanzishwa upya miradi iliyositishwa,itakuwa na madhara yake.Waziri wa kigeni wa Ujerumani,Joschka Fischer wiki iliyopita alisema hatua yo yote ya Iran kuanzisha upya harakati za kinyuklia,kutamaanisha mwisho wa majadiliano.