TEHRAN : Iran iko tayari kwa mazungumzo ya nuklea
23 Agosti 2006Iran imesema hapo jana iko tayari kuwa na mazungumzo makini juu ya mpango wake wa nuklea.
Mpatanishi mkuu wa nchi hiyo juu ya masuala ya nuklea Ali Larijani aliwasilisha jibu la maadishi kwa mabalozi wa Uingereza, China,Russia,Ufaransa,Ujerumani na Switzerland juu ya mpango wa vifuta jasho vya kiuchumi na kisiasa wenye lengo la kuishawishi Iran kusitisha shughuli zake za nuklea.
Larijani amegoma kutaja iwapo jibu lao linajumuisha kukubali kusitisha urutubishaji wa uranium na hakuna ufafanuzi uliotolewa juu ya jibu hilo la Iran.
Televisheni ya taifa imemkariri Larijani akiwaambia wanadiplomasia hao kwamba iko tayari kuanzia leo tarehe 23 mwezi wa Augusti kuingia kwenye mazungumzo mazito na nchi zilizopendekeza mpango huo wa vifuta jasho.
Hata hivyo hakuna dalili kwamba Iran iko tayari kuitikia dai la kusitisha urutubishaji wa uranium ifikapo Augusti 31 au venginevyo kukabiliwa na uwezekano wa kuwekewa vikwazo.