TEHRAN Iran bado yaringa kuhusu mpango wake wa nuklia
6 Juni 2005Afisa wa ngazi ya juu wa Iran amesema kwamba Iran imekubali kwa masharti matakwa ya umoja wa Ulaya kuendelea kusitisha shughuli zake za kuyarutubisha madini ya uranium, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai mwaka huu.
Iran na maafisa wa Ulaya walikubaliana katika mkutano wa kilele uliofanyika mjini Geneva Uswissi mwezi uliopita, kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo juu ya mpango wa nuklia wa Iran, mwezi Agosti mwaka huu.
Mazungumzo hayo yatafanyika baada ya uchaguzi wa rais unaotarajiwa tarehe 17 mwezi huu na baada ya viongozi wa umoja wa Ulaya kutayarisha mapendekezo yao kuhusu ushirikiano wa umoja huo na Iran juu ya mpango wake wa nuklia.
Iran inataka kalenda hiyo ifupishwe na mazungumzo hayo yafanyike mapema, jambo ambalo huenda likawatatiza wanasiasa wa umoja wa Ulaya ambao wamo mbioni kuandaa likizo zao za msimu wa kiangazi.