TEHERAN: Iran yatoa onyo kwa Israel kutoishambulia Syria
14 Julai 2006Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran,ametoa onyo kwa Israel kutoishambulia Syria,huku mashambulio dhidi ya Lebanon yakiendelea.Alipozungumza kwenye televisheni ya taifa alisema,shambulio dhidi ya Syria litatazamwa kuwa ni shambulio dhidi ya ulimwengu mzima wa kiislamu.Rais Ahmedinejad akaongezea kuwa shambulio la aina hilo litajibiwa vikali na akailaumu Israel peke yake kwa mgogoro uliyozuka hivi sasa.Israel kwa upande mwingine inazilaumu Iran na Syria kuwa zinawasaidia wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon.Hali ikizidi kuwa tete katika Mashariki ya Kati,Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamia kukutana kwa kikao maalum leo hii mjini New York.Siku ya Alkhamis,mswada wa azimio wa kutaka kutoa lawama dhidi ya Israel,ulishindwa kupitishwa katika Baraza la Usalama baada ya Marekani kutumia kura yake ya turufu.