Tanzia: Mohammed Abdulrahman, safari iliyowacha alama
17 Julai 2025Jina lake kamili ni Mohammed Abdulrahman Mkufunzi. Ikasadifu kwamba jina la babu yake, Mkufunzi, ambalo linamaanisha fundi anayefundisha wengine, ikawa ndiyo khulka na mwenendo wake kitaaluma na kikazi.
Watangazaji wengi waliopo Idhaa ya Kiswahili ya DW na hata idhaa nyengine za kimataifa ni matokeo ya moja kwa moja ya ukufunzi wake na hawafichi jinsi walivyofundika chini ya ufundi wa 'mkufunzi' huyu.
Bruce Amani aliyejiunga na DW mwaka 2011 anamkumbuka Mohammed kama mtu aliyempokea na kumfundisha kazi kwa ufanisi mkubwa. "Niliwahi kumwambia kuwa nina bahati kuwa njia zetu zimekutana na kwake nimejifundisha kuwa namna hivi nilivyo leo."
Safari iliyowacha alama
Mohammed alijiunga na Deutsche Welle mwaka 1980 akitokea nchini Komoro, ambako alikuwa akifanya kazi kwenye shirika la utangazaji la visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi, chimbuko la wazee wake.
Mwenyewe, hata hivyo, ni mzaliwa wa Tanganyika ya wakati huo (sasa Tanzania Bara) kwa wazazi wenye asili ya Kizanzibari na Kingazija na alikuja baadaye kuhamia kisiwani Unguja kwa masomo na maisha kabla ya kwenda London, Uingereza, kisha Moscow, Urusi, alikosomea uandishi wa habari.
"Mimi asili yangu ni Mngazija, ni Mtanganyika kwa kuzaliwa, Mzanzibari ikiwa ni chimbuko la mama yangu, na Mtanzania kutokana na Muungano wa mataifa mawili ya Tanganyika na Zanzibar 1964. Lakini zaidi najivunia kuwa Mwafrika." Anasema kwenye kitabu alichokichapisha baada ya kustaafu, Maisha Yangu Ninavyoyakumbuka.
Lakini tunapoadhimisha maisha yake baada ya kutangulia mbele ya haki, Mohamed hakumbukwi na wenzake wa DWkwa utambulisho wake huo, bali kwa utambulisho wa kuwa mwandishi bingwa, mahiri na mwenye kipaji cha hali ya juu.
"Kifo cha Mohammed kimenishituwa, kimenifadhaisha sana. Namkumbuka kwa umahiri wake na ukweli kuwa ni yeye aliyekuwa daraja ya mimi kutoka Afrika na kuja hapa kujiunga na DW," anasema Zainab Aziz ambaye alifanya kazi na Mohamed kwa zaidi ya miongo miwili.
Mnyooshaji wa Kiswahili
Miongoni mwa sifa kubwa ambazo Idhaa ya Kiswahili ya DW inajivunia ni msingi wake wa matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, lakini kwa wengi wanafahamu kuwa mjenzi wa msingi huo alikuwa Mohammed.
Josephat Charo aliyekuwa mmoja wa wasaidizi wawili wa mkuu wa Idhaa hii anakumbuka jinsi Mohammed 'alivyowanyooshea lugha' kwenye chumba cha uhariri,
"Ukiwataja watetezi wakubwa wa Kiswahili duniani, Mohammed utamkuta naye yumo. Kwenye mikutano yetu ya uhariri, alikuwa akituelekeza na wakati mwengine hata kutukemea pale anapoona Kiswahili kinatumiwa vibaya. Hakutaka kuona Kiswahili kinachanganywa na lugha nyengine kama vile Kiingereza, kwa mfano." Anaongeza Josephat.
Mohammed alijiunga na DW kama mwanafunzi wa vitendo, akapanda daraja hadi kuwa mtangazaji kamili, akashika wadhifa wa uhariri na hatimaye naibu mkuu wa Idhaa - safari iliyoweka alama ya uandishi, umahiri na wito aliokuwa nao maishani.
Kwake uandishi ulikuwa si sauti tu nyuma ya kipaza sauti cha redio, bali maarifa na muakisiko wa kilimwengu. Ndio maana aliumiliki uandishi na uchambuzi wa masuala ya siasa, michezo na ya kijamii kama vile alivyomiliki hati kwenye maandiko yake.
Huyu ndiye Mohammed Abdulrahman tunayemkumbuka hapa DW.
Innalillahi wainna ilayhir raajiun.
Bwana alitowa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Mola ailaze pema roho ya Mohammed Abdulrahman Mkufunzi.