Tanzania yalaumiwa kwa kukandamiza uhuru wa kisiasa
8 Agosti 2025Taarifa hiyo ya tume ya haki za binadamu pamoja na mambo mengine imevitaja vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika miaka ya hivi karibuni nchini Tanzania kuwa vinaliweka Taifa hilo katika taswira ya uvunjifu wa haki za binadamu.
Baadhi vitendo vilivyotanjwa katika ripoti hiyo ni pamoja na utekaji kwa watu ambao hasa ni wakosoaji wa serikali, na kukamatwa kwa mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu na kufunguliwa kesi ya uhaini kipindi kifupi kuelekea uchaguzi mkuu.
Ripoti hiyo imetaja pia kuzuiliwa kwa wanaharakati mbali mbali kutoka nje ya Tanzania waliokwenda kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu, kuwa kulikiuka Sheria na misingi ya haki za binadamu. Je tamko hili la Tume ya haki za binadamu ya Afrika lina maana gani kisheria? Denis Moses Oulushangai ni mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu.
"Tume ya haki haiwezi ikaibana (Tanzania), lakini tume hiyo inaheshimika sana na katika jumuiya yote ya kimataifa utakuwa unasimangwa na ni aibu, kwa sababu utakuwa unakeuka utaratibu ambao mlijiwekea kama mkataba wa Afrika. Naweza kusema kwamba ni aibu kubwa sana kwa Tanzania", alisema Oulushangai.
Taarifa hiyo iliyoonesha wasiwasi wa ulinzi wa haki za binadamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Taifa hilo unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, pia imetaja kasoro zingine kuwa ni vizuizi vya upatikanaji wa taarifa, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni.
Kuzuiliwa kwa mitandao ya kijamii
Tume hiyo ya Haki ya Afrika imezungumzia kuzuiliwa kwa mtandao wa X pamoja na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii kama vile programu maalumu maarufu ya mazungumzo ya sauti, Clubhouse, mtandao wa YouTube ambapo baadhi ya maudhui hayapatikani na vile vile mtandao wa Telegram, ambavyo vyote haviwezi kupatikana bila kutumia mtandao binafsi wa kidijitali, VPN. Watumiaji wa mitandao na wafuatiliaji wa vyombo vya habari wana maoni gani?
"Mtu anaweza akatoa maoni yake au kuchangia kwenye mjadala wa mtandaoni akaoneka kama anafanya kitu ambacho si sahihi", alisema Vincent.
Hata hivyo Tanzania kupitia wizara ya mambo ya nje ya na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwezi Mei mwaka huu iliwahi kujibu madai kama hayo ya Bunge la Ulaya na kusisitiza kwambaTanzania ni nchi huru inayosimamiwa kwa sheria na kwamba kuingiliwa kati ni kukiuka masuala ya ndani ya nchi.