Tamasha la "Afrika Alive" nchini Ujerumani
24 Januari 2006Muziki wa kabila ya Bakongo ulichezwa wakati wa kufungua rasmi tamasha la “Africa Alive” mjini Frankfurt. Mwimbaji ni Ange Kumbu, mwakilishi maarufu ya sanaa ya Kongo ya Kisasa. Picha zake zinaangaliwa kwenye tamasha hilo. Ange Kumbu alichora picha ya ukimwi, wanasiasa wanaokula rushwa au watoto wanaoishi mitaani ili kuonyesha hali mbaya ya nchi yake baada ya kipindi kirefu cha utawala wa dikteta na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Juu ya sanaa yake anaeleza: “Kwangu mimi, mwakilishi wa sanaa ya kisasa ni kama mwanahistoria anayeandika historia ya nchi yake. Mawazo yangu ninayotoa kutoka maisha ya kila siku na fikra za Wakongo. Sanaa yetu inaonyesha kwa njia yake, nini kinachotokea katika nchi yetu.”
“Africa Alive” ni moja ya tamasha barani Ulaya linaloonyesha sanaa ya Afrika ya kisasa kwa kiasi kikubwa. Kamati iliyoandaa tamasha hilo ilijaribu kuwapa Waafrika wenyewe usemi mkubwa ili waweze kutoa picha ya kuchamgamsha ya bara lao.
Mmojawapo ni Muepu Mwamba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo: "Katika ratiba yetu tulikataa kile kilichojaribu kuwashtua tu wageni, kwa mfano katika filamu. Picha ya Afrika ya ajabu haituvutii. Hatutaki kuweka picha nzuri mno ya Afrika, lakini tunataka kuonyesha hali ilivyo ya bara la Afrika hii leo pamoja na matatizo yake, maafa yake na majaribio ya watu kukimbia maafa. Kwa hivyo tulialika wasanii wengi ili Afrika ipande jukwaa!”
Sanaa muhimu kabisa ya tamasha la “Africa Alive” ni filamu. Filamu nyingi za Kiafrika zinahusu mwenendo wa kiuchumi na kidemokrasi wa bara hilo. Mfano mmoja ni filamu iitwayo “La Nuit de la Vérité” - “Usiku wa ukweli” iliyotengenezwa na mwendeshaji filamu wa Burkina Fasi, Fanto Regina Nacro.
Hadithi ya filamu yake inazungumzia taifa mojawapo barani Afrika ambapo wawakilishi wa makabila mawili wanakutana kufikia makubaliano ya amani baada ya miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wote wawili wanatake amani, lakini baadhi ya wajumbe hawakubali.
Hiyo ndiyo mada ya kisasa kabisa katika nchi jirani ya Burkina Faso, yaani Ivory Coast. Hali yake inamsikitisha sana Georgette Paré, mwigizaji mkuu wa kike katika filamu “La Nuit de la Vérité”: “Nchini Burkina Faso tunaongea zaidi ya lugha 60 na hii pia ni idadi ya makabila. Kama ni Mossi au Samo kwangu ni mamoja tu. Au hivyo niliamini kabla ya kupata habari kutoka nchi nyingine ambapo watu wanafukuzwa kwa sababu wanatokea kabila jingine. Kwa hivyo suala la lugha linaweza kuwa muhimu sana.”
Mwishoni mwa wiki hiki baraza litakalofanyika ambalo linajadili suala la kuchokoza, yaani ikiwa Afrika ilinufaika zaidi chini ya utawala wa ukoloni kuliko sasa. Hapana, anasema Muepu Mwamba aliyelazimishwa kukimbia nyumbani kwake nchini Congo miaka 30 iliyopita: “Hatuwezi tu kuangalia upande wa kiuchumi. Muhimu zaidi ni kuuliza vipi tawala za kikoloni zilitenda heshima ya mtu. Kwa maoni yangu hiyo ndiyo sababu kwa nini nchi za Kiafrika haziendelea. Kwa kuwa tawala za kikoloni zilipiga teke heshima ya watu. Halafu waafrika waliofuata madarakani walifanya hivyo hivyo.”