Takriban watu 61 wauawa katika shambulizi la anga, Darfur
26 Machi 2025Shambulizi hilo limeharibu sehemu kubwa ya soko hilo la kila wiki la Tora lililoko umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa el-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini.
Mjumbe wa UN aonya kuhusu hatari ya Sudani Kusini kurudi vitani
Kundi linalojulikana kama Support Darfur Victims, linalotoa msaada kwa waathiriwa wa mzozo huo wa Darfur, lilisambaza kanda za video zilizoonesha majengo yaliyoteketea pamoja na miili iliyoungua ikiwa imetapaka chini.
Zaidi ya nusu ya waliouawa Darfur ni wanawake
Kulingana na orodha iliyotolewea na msemaji wa uratibu wa kundi hilo linalowasaidia waathiriwa wa Darfur, Adam Rejal, zaidi ya nusu ya waliokufa walikuwa wanawake. Orodha hiyo pia imeonyesha majeruhi 23 na watu saba ambao hawajulikani walipo.
Shambulizi la Darfur latajwa kuwa uhali dhidi ya ubinadamu
Rejal amelitaja shambulizi hilo kama uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukwaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa na kibinadamu pamoja na makubaliano.
Shirika lingine la kutetea haki la Darfur Network for Human Rights, limesema watu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la Tora.
Shirika hilo limeongeza kuwa shambulizi hilo lilifanyika wakati soko hilo lilikuwa na shughuli nyingi na idadi kubwa ya wanawake, watoto na wazee.
Wakati huo huo, shirika la wanasheria linalofuatilia vita nchini Sudan, Emergency Lawyers, limesema mamia ya watu wameuawa.
Jeshi la Sudan lasema raia hawajalengwa
Msemaji wa Jeshi la Sudan Brigadia Jenerali Nabil Abdullah, amesema raia hawakulengwa na akaongeza kuwa madai hayo hayakuwa sahihi na kwamba yanaibuliwa kila wakati jeshi hilo linapotekeleza haki yake ya kikatiba na kisheria ya kukabiliana na shabaha za adui.
Shambulizi la Tora ndilo baya zaidi kutokea
Shambulizi hilo la Jumatatu ndilo baya zaidi kutokea katika vita hivyo vilivyoanza mnamo Aprili 2023 wakati mvutano kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF uliporipuka na kuwa vita vya wazi kote nchini humo.
Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi dhidi ya raia
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema kuwa wanasikitishwa sana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia kote nchini Sudan na akalaani pia mashambulizi yanayoongezeka katika maeneo ya watu wengi mashariki mwa Khartoum.