Watu 200,000 wahudhuria mazishi ya Papa Francis
26 Aprili 2025Viongozi wa dunia, waumini wa kikatoliki wamehudhuria mazishi ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis katika uwanja wa Mtakatifu Petro.
Licha ya uwepo wa marais na wakuu wa nchi, mazishi ya Papa Francis yamehudhuriwa na raia wa kawaida, wafungwa na wahamiaji ambao waliusindikiza mwili wake hadi kwenye Kanisa ambako atazikwa hivi leo.
Kengele za Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro zililia kuashiria mwanzo wa harakati za mazishi ya Papa Francis ambapo uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Vatican umesema takriban watu 200,000 wamehudhuria misa hiyo ya mazishi inayofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Marekani Donald Trumpna mkewe Melania, wa Ufaransa Emmanuel Macron, Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya, Mwanamfalme William wa Uingereza na familia ya Kifalme ya Uhispania na wengineo wengi.
Soma pia: Wakristo kote duniani wamuombea Papa Francis
Maelfu ya waombolezaji wamekusanyika kwenye barabara kuu inayofahamika kama della Conciliazione ambayo ndio inayoelekea kwenye Uwanja wa Vatican wa Mtakatifu Petro huku wakifuatilia misa kwenye televisheni kubwa zilizowekwa kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma, ambako Papa Francis atazikwa baadaye leo Jumamosi na kaburi lake kuandikwa Franciscus.
Waombolezaji wameagizwa kujiepusha na vitendo vya kupeperusha bendera au mabango wakati wa ibada ya misa ya kumuaga Papa Francis.
Papa Francis akumbukwa kama mpenda amani
Makadinali walionekana wakivalia mavazi yao mekundu huku Kadinali Giovanni Battista Re aliyeongoza misa hiyo akimuelezea Papa Francis kama "papa wa watu, mwenye moyo safi, aliyehimiza amani na aliyependa kushirikiana na jamii iliyotengwa, kuwasiliana na moja kwa moja na watu binafsi, aliyekuwa na shauku ya kuwa karibu na kila mtu, na hasa waliokuwa na shida.
Alikumbushia pia falsafa ya Papa Francis ya kuhimiza "mazungumzo ya kina" katika juhudi za kumaliza mizozo inayoendelea kote ulimwenguni.
Soma pia: Waafrika wana matamanio ya Papa kutoka kwao
Kama ishara ya kumuenzi Papa, Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine walikutana kwa mazungumzo waliyoyataja kuwa yenye tija kuhusu namna ya kumazila mzozo wa Urusi na Ukraine. Trump na Zelensky walikuwa hawajakutana ana kwa ana tangu walipolumbana katika ikulu ya White House mwezi Februari.
(Chanzo: Mashirika)