Watu 1,000 wafariki katika maporomoko ya ardhi Sudan
2 Septemba 2025Takriban watu 1,000 wamefariki kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la milima ya Marra, magharibi mwa Sudan na kumwacha mtu mmoja pekee aliyenusurika.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mnamo Agosti 31, baada ya siku kadhaa za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Darfur.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vikosi vya Ukombozi wa Sudan (SLM/A) vinavyodhibiti eneo hilo, kijiji kilichoathirika kimezama kabisa ardhini na juhudi za uokoaji zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na hali ya kijiografia na ukosefu wa vifaa.
SLM/A imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa kuingilia kati haraka ili kusaidia katika kuitoa miili ya wahanga, wakiwemo wanaume, wanawake na watoto na pia kutoa msaada wa dharura kwa manusura wachache waliobaki.
Kijiji hicho kilikuwa kinatumika kama hifadhi kwa wakimbizi wa ndani waliokuwa wakikimbia mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF katika jimbo la Darfur Kaskazini.