Zaidi ya waandamanaji 1,100 wako mikononi mwa polisi Uturuki
24 Machi 2025Kukamatwa kwa Imamoglu kumeibua machafuko mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika miaka mingi. Maandamano yaliyoanza mjini Istanbul ya kupinga kukamatwa kwa Ekrem Imamoglu yalisambaa katika zaidi ya mikoa 55 kati ya 81 ya Uturuki ambapo yalizua mapigano kati ya waandamanaji na polisi wa kutuliza ghasia. Machafuko hayo yamekosolewa pakubwa katika ngazi ya kimataifa.
Imamoglu amekuwa akionekana kuwa mwanasiasa pekee ambaye anaweza kumshinda rais Erdogan. Kiongozi huyo wa upinzani alikamatwa siku kadhaa kabla ya jina lake kuthibitishwa Jumatatu na chama chake cha CHP kuwa ndiye mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2028.
Soma zaidi: Mpinzani wa Erdogan Imamoglu achaguliwa kugombea urais
Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumatatu na chama cha waandishi wa habari cha Uturuki, mamlaka nchini humo ziliwakamata waandishi tisa wa habari walioripoti maandamano hayo yaliyokuwa yamepigwa marufuku kutoka kwenye makazi yao katika miji kadhaa. Ekrem Imamoglu, pamoja na watu wengine 100 walikamatwa kwa shutuma za rushwa na ugaidi. Mahakama mjini Istanbul jana Jumapili ilimpeleka jela meya huyo wakati bado kesi yake ikisubiri kusikilizwa.
Gavana wa Istanbul: Jaribio lolote la kuvuruga utaratibu halitavumiliwa
Mapema leo Jumatatu Gavana wa Istanbul Davut Gul ametoa kauli kupitia jukwaa la X akiwatuhumu waandamanaji hao kwa kuharibu misikiti na makaburi na ameonya kuwa, jaribio lolote la kuvuruga utaratibu halitavumiliwa.
Kutokana na hali nchini humo msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya Guillaume Mercier ametahadharisha kuhusu hali ya demokrasia ya Uturuki.
Mercier amesema, "Kukamatwa mwa Meya Imamoglu na pia waandamanaji kunazidisha maswali ikiwa Uturuki inaendelea kufuata utamaduni wake wa muda mrefu wa demokrasia iliyojiwekea. Kama mwanachama wa baraza la Ulaya na nchi inayotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya, Uturuki inapaswa kufuata maadili ya demokrasia. Haki hizi, haki za maafisa waliochaguliwa, pamoja na haki ya watu kufanya maandamano ya amani zinapaswa kuheshimiwa."
Ujerumani kwa Upande wake imelaani kufungwa kwa meya wa Istanbul na kusema inafuatilia kinachoendelea nchini humo ikiwa na wasiwasi mkubwa. Msemaji wa Kansela Olaf Scholz, Steffen Hebestreit amesema kukamatwa kwa Imamoglu ni jambo lisilokubalika hata kidogo.
Ugiriki kwa upande wake kupitia msemaji wa serikali imeonya pia kuhusu hali ya kisiasa ya Uturuki ikisema kuwa ni ya kutia wasiwasi baada ya kukamatwa kwa Ekrem Imamoglu.