Takriban raia 14 wauawa na RSF nchini Sudan
4 Agosti 2025Kundi hilo la The Emergency Lawyers, lililoorodhesha maasi katika vita hivyo kati ya RSF na jeshi la Sudan, limesema kuwa watu 14 wameuawa katika shambulizi hilo la Jumamosi, na makumi ya wengine kujeruhiwa huku idadi ya raia isiyojulikana wakizuiwa.
Wanamgambo wa Sudan watangaza kuunda serikali sambamba
Kundi hilo limesema waathiriwa waliondoka El-Fasher katika juhudi za kutoroka mashambulizi yanayoongezeka.
Hata hivyo, shirika la habari la AFP halikuweza kuthibitisha mara moja idadi hiyo na taarifa zilizotolewa kwasababu mawasiliano yamekatizwa katika eneo la Darfur pamoja na kwamba waandishi wa habari hawawezi kulifikia eneo hilo.
Shambulizi lafanyika siku mbili baada ya raia kutakiwa kuondoka El- Fasher
Shambulizi hilo katika kijiji kilicho cha Qarni viungani mwa El-Fasher, limekuja siku mbili tu baada ya utawala uliowekwa na kundi la RSF kuwataka raia kuondoka mjini humo na kuwaahidi kuwa watakuwa salama.
Katika hotuba kwa njia ya video, gavana wa Darfur aliyeteuliwa na RSF Al-Hadi Idris, aliwataka wakazi hao kuondoka El-Fasher na kuelekea Qarni, katika eneo la kaskazini magharibi vilipo vikosi vya muungano wa Tasis, na kuwahakikishia usalama wao.
Tasis ni muungano wa kisiasa unaoongozwa na RSF ambao mwishoni mwa mwezi uliopita uliwachagua viongozi wa serikali iliyoko katika mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, Nyala.
Idris amesema washirika wa RSF wangetoa njia salama kwa maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na mji wa magharibi wa Tawila, kama vile ambavyo vikosi hivyo vimeweza kupitisha maelfu ya watu walioondoka El-Fasher katika muda wa miezi sita iliyopita.
Katika siku za hivi karibuni, RSF imefanya mashambulizi yake dhidi ya El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini ambalo imeuzingira tangu Mei 2024 lakini halijaweza kuunyakua kutoka mikononi mwa jeshi.
Maelfu ya watu mjini Tawila wanakabiliwa na mlipuko wa kipindupindu
Huko Tawila, Umoja wa Mataifa umesema mamia kwa maelfu ya watu kwa sasa wanakabiliwa na mlipuko mbaya wa ugonjwa wa kipindupindu baada ya kunusurika mashambulizi ya RSF kwenye kambi za wakimbizi zinazozunguka El-Fasher mnamo mwezi Aprili.
Mara kwa mara, jeshi la Sudan na RSFzimeshtumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia na ushambuliaji wa makombora katika maeneo ya makazi.