Taiwan yasema ndege 45 za China ziliingia anga yake
27 Februari 2025Haya yalijiri ikiwa siku moja tu baada ya Taipei kulaani matumizi wa silaha kwenye mazoezi ya kijeshi cha China kusini mwa kisiwa hicho.
Wizara ya Ulinzi wa Taiwan ilisema ndege hizo pamoja na meli 14 za kijeshi zilionekana majira ya saa sita usiku wa kuamkia Alkhamis (Februari 27).
Soma zaidi: Meli za kijeshi za Marekani zavuka mlango bahari wa Taiwan
China inakichukulia kisiwa hicho kuwa ni sehemu ya mamlaka yake na imetishia kutumia nguvu ikibidi ili kukirejesha kwenye udhibiti wake.
Siku ya Jumatano, Taiwan ilisema China ilifanya mazoezi ya kijeshi ikitumia ndege na meli na kwamba ilitangaza kutumia risasi halisi kwenye eneo lililo umbali wa kilomita 74 kusini mwa kisiwa hicho.
Wizara ya mambo ya kigeni ya China imekataa kusema chochote kuhusu mkasa huo.