Taarifa za uongo za AI zinaweza kuathiri uchaguzi Afrika
25 Februari 2025Sauti ama Video hutengenezwa kwa urahisi sana hata kama uko nyumbani kwa msaada wa akili mnemba, tena bila ya malipo yoyote. Lakini kile ambacho kinaweza kutokea miaka mitano au 10 kuanzia sasa ni cha kutisha, anasema Hendrick Sitting, mkurugenzi wa programu ya vyombo vya habari ya Wakfu wa Konrad Adenauer Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ripoti ya Jukwaa la Uchumi mwaka 2024 ya Global Risk pia imetaja usambazaji wa taarifa kwa kutumia Akili Mnemba kama kitisho namba moja na kulingana na Sitting, mara zote hulenga kudhoofisha misingi ya demokrasia na kuigawanya jamii.
Kwa ushirikiano na Wakfu wa Konrad Adenauer, Karen Allen kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Usalama nchini Afrika Kusini na Christopher Nehring wa taasisi inayoangazia uhalifu wa mitandaoni ya nchini Ujerumani waliandika kuhusu taarifa potofu za AI barani Afrika na Ulaya wakati uchaguzi unapokaribia.
Waligundua taarifa za uongo kwa kutumia akili mnemba kwa kiasi kikubwa zililenga kushambulia na kudhofisha mamlaka na michakato za uchaguzi. Uchunguzi huo aidha imethibitisha kwamba taarifa kama hizi hazichunguzwi kwa kina.
Kulingana na Allen na Nehring, Ulaya na Afrika wanakabiliwa na kitisho cha kufanana.
Soma pia:Mkutano wa Paris washindwa kufikia tamko la pamoja kuhusu AI
Lakini katika mataifa mengi ya Afrika, gharama za kupata huduma za mtandao na mitandao ya kijamii mara nyingi ni ghali sana, na katika baadhi ya maeneo haipatikani kabisa.
Ni kutokana na hilo, Nehring na Allen waligundua kuwa kuna usambazaji kidogo wa taarifa za uwongo, ambapo maudhui ya video au sauti hughushiwa kwa kutumia AI - na kwa bei nafuu.
Migogoro inavyotumiwa kueneza habari za uwongo
Mapigano ya sasa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya vikosi vya serikali ya Kongo na M23 yametumika kama uwanja mzuri wa taarifa potofu na matamshi ya chuki. Katikati ya mzozo unaoongezeka, picha na maudhui ya maandishi yanayohusishwa na akaunti za Rwanda yameathiri maoni ya umma, amesema Allen.
Ikiwa na takribani watumiaji milioni 26 wa mitandao ya kijamii, Afrika Kusini ilitoa uwanja mpana kwa upotoshaji wa habari unaoungwa mkono na AI wakati wa uchaguzi wa bunge wa 2024.
Soma pia:Muongozo wa matumizi ya akili mnemba
Chama kipya kilichoanzishwa cha Umkhonto we Sizwe, kinachoongozwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, kilisambaza video bandia ya Rais wa Marekani Donald Trump, akitangaza kukiunga mkono chama hicho. Kulingana na utafiti wa Nehring na Allen, haya yalikuwa maudhui ya AI yaliyosambazwa zaidi wakati wa uchaguzi, na sio tukio la kwanza la uwongo wa kina kuhusu mabadiliko ya mamlaka ya kisiasa.
Nchini Burkina Faso, video zilizosambaa baada ya mapinduzi ya Septemba 2022, ambapo Kapteni Ibrahim Traore alichukua udhibiti, zilikuwa zinawataka raia kuunga mkono utawala wa kijeshi.
Ni bahati mbaya video hizo ghushi, zilizogunduliwa kwa mara ya kwanza kwenye Facebook na kusambazwa kwenye makundi ya WhatsApp na mitandao ya kijamii, zilionyesha watu wanaojiita Pan-Africanists, wanaodaiwa kuwa na mafungamano na mamluki cha Urusi, Wagner, hazikuthibitishwa.
Allen anasema watu barani Afrika wanaweza kujilinda dhidi ya ghiliba mtandaoni kwa kupata habari kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Lakini hili limekuwa gumu kwa sababu majukwaa makubwa ya mitandao ya kijamii kama X na Facebook yameacha kuangalia ukweli kwenye majukwaa yao, na kuwaachia watumiaji jukumu hilo.
Ingawa tafiti zinaonyesha kuwa mazingira ya udhibiti barani Afrika yanayobadilika yanamaanisha kuwa inaweza kujifunza kutokana na makosa yaliyofanywa mahali pengine ili kukabiliana vyema na taarifa potofu zinazotumia AI.
Soma pia:Guterres ashitushwa na Israel kutumia akili bandia Gaza