Syria yaahidiwa zaidi ya dola bilioni 6 za ujenzi mpya
18 Machi 2025Viongozi wapya wa Syria, wakiongozwa na kamanda wa zamani wa waasi Ahmed al-Sharaa, wamekuwa wakitafuta msaada kusaidia kulifufua taifa hilo lililoharibiwa vibaya. Hata hivyo ahadi za mkutano wa Brussels zilitarajiwa kuwa chini kuliko miaka iliyopita.
Jamii ya kimataifa imeahidi zaidi ya dola bilioni 6 kama msaada wa kusaidia ujenzi mpya wa Syria kufuatia uharibifu uliosababishwa na miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Yuro bilioni 4 ni msaada na bilioni moja mkopo
Haya ni kwa mujibu wa Kamishena wa Umoja wa Ulaya Dubravka Suica katika mkutano wa uchangishaji fedha uliofanyika mjini Brussels.
"Unajua Umoja wa Ulaya na nchi zake wanachama, wanasalia kuwa wafadhili wakubwa kufikia sasa wakiwakilisha robo tatu ya ahadi zilizotolewa. Ila kwa sasa ninatangaza kuwa kwa pamoja tumeahidi kutoa jumla ya yuro bilioni 5.8," alisema Suica.
Kulingana na Suica yuro bilioni 4.2 ya ahadi hizo ni fedha zitakazotolewa kama msaada huku dola bilioni 1.6 zikitolewa kama mikopo.
Mawaziri wa Ujerumani, wa mambo ya kigeni Annalena Baerbock na mwenzake wa maendeleo Svenja Schulze, wametangaza yuro milioni 300 za kusaidia suala la misaada ya kiutu, mashirika ya kiraia na elimu, huku fedha hizo pia zikilenga kuwasaidia wakimbizi wa Syria na jamii zinazowahifadhi nchini Jordan, Lebanon, Irak na Uturuki.
Taarifa ya kando ya serikali ya Ujerumani iliyotolewa kwa waandishi wa habari imesema, utekelezaji wa hatua zote hizo utafanywa kupitia mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali na wala sio serikali ya mpito ya Syria.
Marekani kwa upande wake haikutoa ahadi yoyote ila imesema tu kuwa itaendelea kutoa msaada. Wawakilishi wa utawala wa Rais Donald Trump pia wameyataka mataifa mengine sasa kuchukua jukumu la mzigo wa fedha ambalo Marekani imekuwa ikiubeba.
Mataifa ya Magharibi yanapunguza utoaji wa fedha za misaada kwa ajili ya kutumia fedha hizo katika bajeti zao za ulinzi.
Mkutano uliopangwa kwa haraka
Mkutano huo uliofanyika Brussels ulikuwa wa tisa na wa kwanza tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad mwezi Disemba.
Mawaziri na wawakilishi kutoka kwa washirika wa Syria kutoka nchi za Magharibi, mataifa mengine ya Kiarabu na mashirika ya Umoja wa Mataifa, yalihudhuria mkutano huo wa siku moja.
Mkutano huo ulipangwa kwa haraka na Umoja wa Ulaya kutokana na mabadiliko yanayofanyika nchini Syria.
Viongozi wapya wa Syria wanajaribu kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yamegawika katika vijitaifa vidogo vidogo visivyo rasmi, wakati wa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Viongozi hao vile vile wanajaribu kuujenga uchumi pamoja na miundo mbinu. Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa dola bilioni 250 ndizo zitakazohitajika kuijenga upya Syria huku wataalam wakisema kiwango hicho kinaweza kufikia dola bilioni 400.
Vyanzo: DPAE/APE