Swichi za mafuta zilizimwa kabla ya ajali ya Air India
12 Julai 2025Ripoti hiyo, iliyotolewa leo na Ofisi ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege ya India, AAIB pia imeeleza kuwa rubani mmoja alisikika kupitia kinasa sauti cha chumba cha marubani akimuuliza mwenzake kwanini alikatiza mafuta kwenye ndege katika dakika za mwisho mwisho kabla ya ndege kuanguka, lakini akajibu kuwa hakufanya hivyo.
Ripoti hiyo ilizingatia matokeo yake kwenye data iliyopatikana kutoka kwa visanduku vyeusi vya ndege hiyo ambavyo hunasa sauti za marubani na kurekodi data za safari ya ndege.
Ndege hiyo ya Air India aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ilianguka mnamo Juni 12 na kuwauwa takriban watu 260 ikiwa ni pamoja na wengine 19 waliokuwa katika eneo ilikoanguka kwenye mji wa Ahmedabad kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Ni mtu mmoja tu aliyenusurika ajali hiyo ambayo ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea katika sekta ya safari za angani nchini India.
Ripoti hiyo haikubaini ni kauli zipi zilizotolewa na rubani mkuu na zipi zilitolewa rubani msaidizi, au ni rubani yupi aliyetoa ujumbe wa dharura wa "Mayday, Mayday, Mayday" kabla ya kuanguka.
Rubani kinara wa ndege hiyo ya Air India alikuwa Sumeet Sabhrwal, 56, ambaye alikuwa na uzeofu wa kurusha ndege kwa saa 15, 638, na kwa mujibu wa serikali ya India, alikuwa pia mkufunzi wa shirika la Air India.
Msaidizi wake alikuwa Clive Kunder, 32, ambaye alikuwa na uzoefu wa kuwa angani kwa jumla ya saa 3,403.
Ripoti ya uchunguzi huo wa awali haikusema ni vipi swichi hizo zilizima wakati wa safari hiyo.
Watalaamu wanasema rubani asingeweza kuzizima swichi hizo kwa bahati mbaya.
Ajali hiyo ni changamoto kwa malengo ya kampeni ya kampuni ya Tata Group kurejesha hadhi ya Air India na kuimarisha ndege zake, baada ya kulinunua shirika hilo kutoka kwa serikali mwaka wa 2022.
Air India imeikubali ripoti hiyo na kusema katika taarifa kuwa inashirikiana na maafisa wa India katika uchunguzi wao lakini ikakataa kutoa kauli zaidi.
Bodi ya Kitaifa ya Marekani ya Usalama wa Usafiri iliwashukuru maafisa wa India kwa ushirikiano wao katika taarifa na ikabainisha kuwa hakukuwa na hatua zinazopendekezwa katika ripoti hiyo zinazowalenga waendeshaji wa ndege za Boeing 787 au injini za GE.
Kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing imesema inaendelea kuunga mkono uchunguzi huo na mteja wake Air India.
afp, dpa, ap, reuters