Sweden yakamata meli inayoshukiwa 'kuhujumu' nyaya za Baltic
27 Januari 2025Latvia ilipeleka meli ya kivita kuchunguza kitendo hicho cha hivi karibuni cha hujuma. Taarifa kutoka ofisi ya Mwendesha mashitaka wa Sweden imesema wameanzisha uchunguzi kuhusu hujuma hiyo. Jeshi la wanamaji la Latvia awali lilisema lilitambua "meli inayoshukiwa" kufanya kitendo hicho ya Michalis San, karibu na eneo la tukio pamoja na meli nyingine mbili.
Kitendo hicho cha hivi karibuni kimejiri wakati mataifa yanayozunguka Bahari ya Baltic yakihangaika kuimarisha ulinzi wao baada ya tuhuma za hujuma ya nyaya za chini ya bahari katika miezi ya hivi karibuni, huku baadhi ya waangalizi wakiilaumu Urusi. Waziri Mkuu wa Latvia Evika Silina amesema amewasiliana na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson kuhusu tukio hilo. Sweden, Latvia na Jumuiya ya Kujihami NATO wamashirikiana kwa karibu katika uchunguzi.