Sudan yakabiliwa na mgogoro mbaya kabisa wa kibinadamu
11 Aprili 2025Vita vilivyodumu karibu miaka miwili vimeitumbukiza Sudan katika mgogoro mbaya kabisa wa kibinadamu na kuifanya nchi hiyo ya Afrika kuwa taifa pekee linalokabiliwa na baa la njaa. Hayo yamesemwa hivi leo na afisa wa cheo cha juu wa Umoja wa Mataifa.
Mratibu wa masuala ya dharura wa shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan Shaun Hughes amesema karibu watu milioni 25 wanakabiliwa na njaa huku watu wakifa katika maeneo yanayokabiliwa na njaa huko Darfur Magharibi.
Akizungumza na maripota wa Umoja wa Mataifa, afisa huyo pia amesema kwa kipimo chochote hili ndilo janga kubw kabisa la kibinadamu duniani, akitaja zaidi ya watu milioni nane waliolazimika kuyakimbia makazi yao nchini Sudan na milioni nne waliovuka mpaka kukimbilia nchi saba ambazo pia zinakabiliwa na njaa na zinahitaji msaada wa kibinadamu.