Sudan yaishtaki UAE kwenye mahakama ya ICJ
7 Machi 2025Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Haki imesema kesi ya Sudan iliyowasilishwa jana, imejikita kwenye matendo inayodai yamefanywa na kundi la RSF, ikiwemo mauaji ya halaiki, wizi wa mali, ubakaji, kuwalazimisha watu kukimbia, uharibifu wa mali za umma na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya jamii ya watu wa Masalit.
Kwenye kesi hiyo, Sudan inaituhumu UAE kuwa mhusika kwenye matendo hayo, kupitia uungaji wake mkono wa moja kwa moja wa kifedha, kisiasa na kijeshi kwa kundi la RSF.
Soma pia: UN yaonya juu ya kuundwa kwa serikali ya amani nchini Sudan
Umoja wa Falme za Kiarabu umeitaja kesi hiyo kuwa mbinu ya Sudan "kujisafishia jina mbele ya umma na kwamba haina ukweli wala msingi wowote wa kisheria."
RSF na jeshi la Sudan wamekuwa wakipambana kwa karibu miaka miwili sasa kuwania madaraka na kila upande umekuwa ukiutuhumu mwingine kufanya uhalifu dhidi ya binaadamu.