Sudan: Watu 158 wafariki kwa kipindupindu huko Darfur
24 Agosti 2025Wizara ya afya katika jimbo hilo linalodhibitiwa na wanamgambo wa RSF imesema vifo hivyo vimeripotiwa kuanzia mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu. Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema mlipuko wa kipindupindu huko Darfur ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi nchini Sudan na unatishia kuenea hadi katika nchi jirani za Sudan Kusini na Chad.
Zaidi ya miaka miwili ya mapigano kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF yamepelekea sehemu kubwa ya Darfur kusalia bila msaada wa bidhaa muhimu. Umoja wa Mataifa umetahadharisha pia kuhusu hali mbaya ya kibinaadamu karibu na mji mkuu uliozingirwa wa jimbo la Darfur Kaskazini wa El-Fasher. Kipindupindu ni maambukizi makali ya utumbo ambayo huenea kupitia chakula na maji vilivyochafuliwa na bakteria.