Sudan kuunda serikali mpya baada ya kuidhibiti Khartoum
10 Februari 2025Vyanzo vya kijeshi nchini Sudan vimeeleza kuwa serikali mpya inatarajiwa kuundwa baada ya kudhibitiwa kikamilifu kwa mji mkuu wa Khartoum, vikikariri taarifa iliyotolewa siku moja kabla na mkuu wa kijeshi Abdel-Fattah al-Burhan.
Burhan aliuambia mkutano wa wanasiasa wanaoegemea jeshi katika ngome ya kijeshi huko Port Sudan siku ya Jumamosi kwamba, serikali mpya ya muda au serikali ya wakati wa vita itakayoundwa, itasaidia kukamilisha malengo ya kijeshi yaliyosalia ya kuikomboa Sudan kutoka kwa waasi.
Jeshi la Sudan ambalo limekuwa katika vita na wanamgambo wa RSF, limepata mafanikio katika wiki za hivi karibuni kuelekea mji mkuu wa Khartoumpamoja na maeneo mengine. Vikosi vya RSF, vimerudi nyuma vikizidiwa nguvu na uwezo wa anga wa jeshi uliopanuliwa na safu za ardhini.