Sudan Kusini yasema Machar alijaribu kuchochea uasi
29 Machi 2025Serikali ya Sudan Kusini imesema hapo jana kwamba Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar aliyekamatwa wiki hii, atachunguzwa kwa madai ya kujaribu kuchochea uasi.UN yaelezea hofu ya Sudan Kusini kurejea katika vita
Msemaji wa serikali na waziri wa habari Michael Makuei alisema katika taarifa yake kwamba Machar na wenzake kutoka chama cha SPLM/A-IO, ambao wamekamatwa siku ya Jumatano, wanachunguzwa na watafikishwa mahakamani.
Waziri huyo amemshutumu Machar kwa kuwahimiza wafuasi wake na kuwachochea kuasi serikali kwa lengo la kuvuruga amani ili uchaguzi usifanyike na Sudan Kusini irudi vitani.
Ripoti za kukamatwa kwa Machar, mpinzani wa muda mrefu wa Rais Salva Kiir, zimechochea wito wa kimataifa wa kujizuia ili nchi hiyo isirejee tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Nchi jirani ya Kenya tayari imemtuma waziri mkuu wake wa zamani, Raila Odinga, kutuliza mvutano.