Sudan: Je, vita vya umwagaji damu vinaelekea kufikia mwisho?
6 Februari 2025Kusonga mbele hivi karibuni kwa Jeshi la Sudan, SAF, dhidi ya wanamgambo wa Rapid Support Forces, RSF katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na mji wa karibu wa Omdurman kunaashiria mabadiliko ya mkwamo mbaya ya umwagaji damu ambao umetawala kwa miezi kadhaa iliyopita katika vita vya Sudan.
Wiki iliyopita, Jenerali Abdel-Fattah Burhan, anayeongoza jeshi la serikali, alirejea kwenye makao makuu mjini Khartoum kwa mara ya kwanza ikiwa ni takribani miaka miwili. Mapema Januari, jeshi la serikali lilifanikiwa kuukomboa mji muhimu wa kimkakati wa Wad Madani, ambao uko umbali wa kilomita 180 kusini kwa Khartoum.
Hager Ali, mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Masomo ya Kimataifa ameiambia DW kuwa Wad Madani ilipoangukia kwenye vikosi vya RSF Desemba, mwaka 2023, nchi nzima ilikumbwa na mshtuko. Hager anasema Wasudan walipoteza matumaini na uwezo wa vikosi vya Sudan, na ndiyo maana kuzingirwa kwa Wad Madani kumebaki kwenye kumbukumbu ya watu. Anasema RSF iliathiri sekta ya kilimo, na kwamba huo ulikuwa wakati ambapo uhaba wa chakula ulizidi kuwa mbaya.
''Ukichoma mazao, ukiharibu mashamba na vifaa vya kilimo, kimsingi unaharibu uwezo wa watu kujikimu. Ndiyo maana huo ulikuwa wakati muhimu.''
Kutokana na kuharibika kwa miundombinu muhimu katikakati mwa jiji, umuhimu wa kimbinu na kimkakati ambao Wad Madani ulikuwa nao mwaka mmoja uliopita kama mji unaotegemewa kwa uzalishiji wa chakula, pia unakaribia kutoweka.
Darfur kama uwanja wa vita unaofuata na wa mwisho?
Tangu RFS ilipopoteza udhibiti wa Wad Madani, wapiganaji wake walirudi nyuma hadi kwenye jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan, ambako RSF inadhibiti wilaya nne kati ya tano.
Osman Mirghani, mhariri mkuu wa gazeti la Sudan la Al-Tayar, ameiambia DW kuwa muda wa kuelekea mwishoni mwa vita umewadia, uwanja wa mapambano umehamia El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini. El Fasher umekuwa chini ya RSF tangu mwezi Mei, mwaka 2024.
Soma pia: Serikali ya Sudan yalaani vikwazo dhidi ya al-Burhan
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, hali ya kiutu Darfur sasa imekuwa mbaya sana. Takribani watu milioni 1.6 wameyakimbia makaazi yao kutoka jimbo la Darfur Kaskazini pekee, watu wapatao milioni mbili wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku watu 320,000 tayari wanakumbwa na baa la njaa.
Raia wa Sudan nchi nzima wamekuwa wakibeba mzigo mkubwa wa mzozo huo, ambao ulizuka Aprili 2023 wakati Jenerali Abdel-Fattah Burhan alipokosana na aliyekuwa makamu wake, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, kuhusu kujumuishwa kwa wanamgambo wa RSF katika jeshi la kawaida.
Wiki hii, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk alionya kuwa ''vita visivyo na maana'' vimekuwa hatari zaidi kwa raia. Matamshi hayo ameyatoa kufuatia shambulizi la mwishoni mwa juma lililopita, ambapo RSF iliwaua takribani raia 54 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 160 katika soko moja huko Omdurman. Siku chache kabla, watu wasiopungua 70 waliuawa katika shambulizi la RSF kwenye hospitali moja huko El Fasher.
Vikwazo na uhalifu wa kivita
Wakati huo huo, baada ya takribani miaka miwili ya kutolewa onyo, mojawapo ya hatua za mwisho za utawala ulioondoka wa Marekani chini ya Joe Biden, ilikuwa ni kuwawekea vikwazo majenerali wote wawili. RSF chini ya Jenerali Dagalo ilishutumiwa kwa mauaji ya kimbari, pamoja na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Nalo jeshi la serikali ya Sudan chini ya Jenerali Burhan, lilishutumiwa kwa kufanya mashambulizi mabaya dhidi ya raia na kudhoofisha lengo la kipindi cha mpito cha kidemokrasia.
Hata hivyo, Leena Badri, mtafiti katika taasisi ya wachambuzi ya Chatham House yenye makaazi yake mjini London, Uingereza ameiambia DW kuwa hana matumaini sana kwamba shinikizo la Marekani pekee linaweza kuwasukuma majenerali wanaohasimiana kuvimaliza vita hivyo.