Sudan inaituhumu UAE kutumia droni kushambulia Port Sudan
21 Mei 2025Hapo jana, jeshi la Sudan lilitangaza kulikomboa eneo lote la Greater Khartoum baada ya kuwafurumusha wanamgambo wa mwisho wa RSF waliokuwa wamebaki katika eneo muhimu kwao la Omdurman. Hatua hii ni mafanikio makubwa zaidi kwa jeshi la Sudan ndani ya karibu miezi miwili, na imethibitisha upya udhibiti wake wa mji mkuu, Khartoum na maeneo jirani. Msemaji wa Jeshi la Sudan, Brigedia Jenerali Nabil Abdallah alitangaza kuwa jimbo la Khartoum sasa "limeondolewa kabisa kwa waasi," akimaanisha kikosi cha RSF ambacho kimekuwa kikipambana na jeshi tangu Aprili 2023.
"Leo tunatangaza kuwa jimbo la Khartoum limeondolewa mikononi mwa wanamgambo wa kigaidi wanaoongozwa na Dagalo. Mji mkuu wetu umesafishwa dhidi ya waasi na wanaowaunga mkono. Tunathibitisha kuwa Khartoum sasa haina tena wahalifu hao, na tunarudia ahadi yetu kwa watu wa Sudan: tutaendeleza juhudi zetu hadi pale waasi, wasaliti, na mawakala wa kigeni watakapoondolewa katika kila kipande cha nchi yetu,'' alisema brigedia Jenerali Nabil Abdallah.
Mapigano makali yazuka kati ya jeshi la Sudan na RSF
Awali jeshi lilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi kuwaondoa wapiganaji wa RSF kutoka maeneo ya Salha na Ombada walikokuwa wamebaki. Mafanikio haya yanatokea katikati ya vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, ambapo watu zaidi ya milioni 13 waliyahama makazi yao, na hali ambayo Umoja wa Mataifa umeitaja kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani na ambalo limeathiri hasa maeneo kama Darfur na Khartoum.
Umoja wa Afrika wapongeza uteuzi wa Waziri Mkuu mpya Sudan
Katika juhudi za kuonesha sura ya uongozi wa kiraia katikati ya mgogoro huo, Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alimteua Kamil al-Taib Idris, kuwa waziri mkuu.
Hatua hiyo imepokelewa vyema na Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, huku Umoja wa Afrika ukisema ni "hatua kuelekea utawala shirikishi." Burhan pia aliwateua wanawake wawili kujiunga na Baraza la Uongozi la Mpito na kulipokonya baraza hilo baadhi ya mamlaka yake, hatua ambazo zinaonekana kuwa dalili ya kuelekea utawala wa kiraia.
Kamil Idris ateuliwa waziri mkuu mpya wa Sudan
Licha ya ushindi wa kijeshi, mashambulizi ya RSF, yakiwemo ya droni, yameendelea kulenga miundombinu muhimu katika maeneo ya serikali, na kusababisha kukatika kwa maji na umeme, hali iliyochochea janga la mlipuko wa kipindupindu uliowaua watu 51 kati ya visa zaidi ya 2,300 vilivyotokea ndani ya kipindi cha wiki tatu zilizopita wengi wao wakiwa mjini Khartoum. Aidha, janga la kibinadamu linaendelea kuwa baya zaidi kufuatia wimbi kubwa la wakimbizi wa ndani.
Wakati huo huo, Sudan imeushutumu Umoja wa Falme za Kiarabu UAE kwa kushambulia bandari ya Port Sudan kwa kutumia droni, madai ambayo UAE imekanusha. Katika hali hii ya mzozo unaoendelea, Sudan imeusihi Umoja wa Afrika kurejesha uanachama wake, ikisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha amani na uthabiti, japokuwa nchi hiyo bado inasalia kwenye mgawanyiko wa kisiasa na mapigano makali kati ya jeshi na wapiganaji wa RSF.
ap/reuters/afp