Steinmeier akutana na Mohammed bin Salman mjini Riyadh
4 Februari 2025Steinmeier alilakiwa kwa heshima za kijeshi kabla ya kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa Saudi Arabia yalioangazia mustakabali wa Syria baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad pamoja na hali katika Ukanda wa Gaza kufuatia kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas.
Mada zingine zilijumuisha serikali mpya ya Marekani chini ya Rais Donald Trump na ushawishi wa Iran.
Ujerumani na Saudi Arabia zaunga mkono suluhisho la mataifa mawili
Ujerumani na Saudi Arabia zinaunga mkono kwa pamoja suluhisho la mataifa mawili kwa Israeli na Palestina. Pia zimejitolea kuleta utulivu Syria, ambayo kiongozi wake wa mpito Ahmed al-Sharaa alikuwa mjini Riyadh siku ya Jumapili.
Israel na Hamas zabadilishana wafungwa kwa mateka
Steinmeier ni rais wa kwanza wa Ujerumani kuizuru Saudi Arabia. Awali ziara hiyo ilipangwa kufanyika mwezi Novemba, lakini iliahirishwa baada ya kusambaratika kwa muungano wa vyama vitatu vya kansela Olaf Scholz.
Kutoka Saudi Arabia, rais huyo wa Ujerumani ataelekea Jordan leo ambapo anatarajiwa kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani katika kambi ya jeshi la anga huko al-Azraq.
Steinmeier kukutana na mfalme Abdulla wa pili wa Jordan
Kesho Jumatano, Steinmeier atafanya mazungumzo na mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan huko Amman ili kujadili hali katika kanda hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, Jordan imewachukuwa mamia ya maelfu ya wakimbizi kutoka taifa jirani la Syria.
Huku hayo yakijiri, Israel inajiandaa kupeleka ujumbe wa ngazi ya juu katika mji mkuu wa Qatar, Doha, kujadili kuendelezwa kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Haya yamesemwa leo na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Kundi la Hamas liko tayari kwa awamu ya pili ya mazungumzo
Kundi la Hamas limesema liko tayari kwa awamu ya pili ya mazungumzo hayo ya amani yanayosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani.
Mazungumzo hayo ya awamu ya pili kuwezesha kusitishwa kabisa kwa vita, yanatarajiwa kuanza hii leo.
Netanyahu kukutana na Trump hii leo
Katika hatua nyingine, mgogoro wa Mashariki ya Kati ndio utakaoongoza ajenda ya leo wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, atakapokutana na Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kiongozi huyo kurejea tena madarakani kwa muhula wa pili.
Netanyahu aliwasili Marekani Jumapili jioni.
Netanyahu kujadili na Trump "ushindi dhidi ya Hamas"
Katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon, amesema kuwa mkutano kati ya viongozi hao wawili ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kina kati ya Israel naMarekani.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, Trump na Netanyahu pia wanatafuta kupiga hatua za kuelekea makubaliano ya kurekebisha mahusiano kati ya Israel na Saudi Arabia.