Starmer: Putin hana budi kuketi kwenye meza ya mazungumzo
15 Machi 2025Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amebainisha kuwa suala la kusitisha vita Ukraine sasa liko mikononi mwa Urusi, na kuwa Rais Vladimir Putin hana budi kuketi katika meza ya mazungumzo. Starmer ameyasema hayo baada ya mkutano wake na viongozi wengine wa mataifa yanayoiunga mkono Ukraine.
Zaidi Starmer aliyeuitisha mkutano huo amesisitiza kuwa, mipango yoyote ya kuweka silaha chini kati ya Ukraine na Urusi ni lazima ihusishe juhudi za Marekani. Ameongeza kuwa, wakuu wa majeshi wa nchi zenye utayari wa kuisaidia Ukraine watakutana Uingereza kuzungumzia mipango ya kuwa na ujumbe wa amani nchini humo ili kuyalinda makubaliano yoyote ya kusitisha vita yatakayopatikana.
Soma zaidi.Shambulio la Israel limewauwa watu 9 mjini Beit Lahiya Ukanda wa Gaza
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliyeshiriki pia kwenye majadiliano hayo ameitolea wito Urusi kufanya juhudi ili kurejesha amani Ukraine, baada ya miaka mitatu ya vita. Naye Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema amani inapaswa kurejeshwa bila masharti yoyote.