Starmer, Merz kusaini mikataba ya ulinzi na biashara
17 Julai 2025Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer na Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz wanajiandaa kusaini mkataba wakiahidi kuimarisha uhusiano katika masuala ya ulinzi na kuongeza ushirikiano wa utekelezaji wa sheria dhidi ya magenge yanayosafirisha wahamiaji kinyume na sheria kuvuka ujia wa bahari ya Atlantiki, English Channel unaolitenganisha eneo la kusini mwa England na kaskazini mwa Ufaransa.
Mkataba huo unaendeleza mkataba wa ulinzi ambao Uingereza na Ujerumani, nchi mbili zenye uchumi mkubwa Ulaya zinazoiunga mkono Ukraine, zilitiliana saini mwaka uliopita zikiahidiana ushirikiano wa karibu katika kukabiliana na kitisho cha Urusi.
Ujerumani na Uingereza zinatarajiwa pia kusaini mikataba kadhaa ikiwemo ya uwekezaji, biashara na uhamiaji.
Kansela Merz yuko jijini London katika ziara yake ya kwanza rasmi ya siku tatu nchini Uingereza tangu alipoingia madarakani mnamo mwezi Mei mwaka huu.