Starmer akutana na Zelenskyy kabla ya mkutano wa Alaska
14 Agosti 2025Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amemkaribisha hii leo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ofisini kwake, Mtaa wa Downing mjini London, katika kile kinachoonekana kama ishara ya Uingereza kuiunga mkono Kyiv siku moja kabla ya mkutano huo muhimu kati ya Marekani na Urusi huko Alaska.
Zelensky anazuru mji huo mkuu wa Uingereza siku moja baada ya kushiriki kwenye mazungumzo kwa njia ya mtandao huko mjini Berlin, Ujerumani, pamoja na Rais wa Marekani Donald Trump na viongozi wa baadhi ya mataifa ya Ulaya.
Kulingana na Ikulu ya Kremlin hii leo, mkutano huo wa Putin na Trump utaanza majira ya saa tano za asubuhi kwa saa za eneo hilo. Mshauri wa sera za kigeni Yuri Ushakov amewaambia waandishi wa habari kwamba Putin na Trump watakutana kwanza kwa mazungumzo ya ana kwa ana na kufuatiwa na mkutano kati ya wajumbe wa pande hizo mbili, kisha mazungumzo yataendelea kwenye "staftahi ya kikazi"
Putin asifu dhamira ya Marekani ya kupata suluhu nchini Ukraine
Putin mapema leo alifanya mkutano na maafisa wa ngazi za juu wa serikali na maafisa wa usalama kuhusiana na mkutano huo. Kwenye video iliyochapishwa na Kremlin, kiongozi huyo ameisifu serikali ya Trump kwa jitihada zake za kuumaliza mzozo huu kwa amani.
"Ningependa kuwashirikisha mahali tulipo hivi sasa na serikali ya Marekani.. na kama kila mtu anavyojua vizuri, inafanya.... kwa maoni yangu, juhudi kubwa na za dhati za kusitisha uhasama, kumaliza mgogoro na kufikia makubaliano yatakayonufaisha pande zote mbili kwenye mzozo huo."
Putin pia alipendekeza kwamba wanaweza kufikia makubaliano na Marekani juu ya udhibiti wa silaha za nyuklia.
Mjini Kyiv, taarifa zinasema Ukraine na Urusi zimefanya mabadilishano mengine ya wafungwa hii ikiwa ni kulingana na Rais Zelenskyy. Kiongozi huyo, ameushukuru Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kusaidia kuratibu awamu hii ya mabadilishano ambayo ni ya 67 tangu kuanza kwa vita hivyo. Kyiv imesema wanajeshi wake 33 na raia 51 walirudishwa nyumbani.
Urusi pia imethibitisha kuwapokea wanajeshi wake na kulingana na Wizara ya Ulinzi wafungwa 84 wamerejea.