Starmer afanya ziara ya kukutana na Trump Washington
27 Februari 2025Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer anafanya ziara nchini Marekani leo akiwa na matumaini ya kumshawishi Rais Donald Trump kuwa amani ya kudumu nchini Ukraine itapatikana pale serikali mjini Kyiv na viongozi wa Ulaya watakapokuwa sehemu ya mazungumzo na Urusi.
Ziara hiyo ya Starmer ambayo inafanyika siku chache baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuitembelea Washington, inadhihirisha wasiwasi unaoongezeka barani Ulaya juu ya mpango wa Trump wa mazungumzo na Urusi kuhusu vita vya Ukraine.
Viongozi wa bara hilo wana mashaka kwamba shinikizo la Trump la kuharakisha mazungumzo hayo litatoa mwanya wa kukubaliwa kupita kiasi matakwa ya Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Vilevile wameingiwa hofu na uamuzi wa Trump wa kufanya mashauriano ya awali na Urusi wiki iliyopita bila kuishirikisha Ukraine au mataifa ya bara hilo.