Smart Class Zanzibar: Mapinduzi ya kidijitali shuleni
1 Septemba 2025Zanzibar sasa imejiunga rasmi na ulimwengu wa masomo ya kidijitali kupitia teknolojia ya Smart Class, maarufu kama darasa janja – na mabadiliko yake yanaonekana wazi.
Ndani ya Shule ya Sekondari Tumekuja, wanafunzi sasa wanasoma kwa mtindo wa kisasa kabisa. Kwa msaada wa skrini kubwa ya kidijitali na kompyuta, walimu wanaweza kufundisha madarasa kadhaa kwa wakati mmoja, kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu na kuhakikisha mitaala inakamilika kwa haraka.
"Kupitia darasa hili la kisasa, wanafunzi wanapata ujuzi wa TEHAMA unaowawezesha kujitegemea hata kama hawapati ajira rasmi. Ndiyo maana shule yetu sasa inaitwa shule ya nyota tano,” anasema Dk. Suleiman Salum Abdallah, mkuu wa shule hiyo.
Mageuzi haya ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Zanzibar wa kuwekeza kwenye elimu na miundombinu ya kisasa.
Faida za Smart Class
Bajeti ya elimu imeongezeka kutoka bilioni 265 mwaka 2023 hadi bilioni 860 mwaka 2025.
Zaidi ya kompyuta 3,000 zimesambazwa, shule mpya 35 zimejengwa, na shule nyingine 25 zinatarajiwa kufunguliwa mwaka huu.
Kwa sasa, kati ya shule za umma 600, tayari 80 zimewekewa vifaa vya TEHAMA, na mpango ni kuongeza madarasa janja katika shule nyingine 20 kabla ya mwisho wa 2025.
Matokeo ni ya kushangaza: ufaulu wa kidato cha sita umefikia 99.8%, wanafunzi hawatoroki tena shule, na ari ya kusoma imeongezeka maradufu.
Walimu pia wamejipanga kuhakikisha hakuna tena wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na "division tatu au sifuri”.
Licha ya changamoto ya umeme, suluhu ipo. Shule nyingi sasa zinaanza kuwekeza kwenye nishati ya jua huku Wizara ya Elimu ikiahidi kushirikiana kuhakikisha mfumo huu wa masomo ya kidijitali unakua bila vikwazo.
Smart Class sio tu mageuzi ya elimu; ni uwekezaji katika kizazi kipya cha kidijitali, kinachoandaliwa kuongoza Zanzibar na dunia katika enzi ya teknolojia.